Magoli ya wachezaji John Bocco na Mrisho Ngassa yamedhihirisha kukua kwa kiwango cha Azam FC baada ya kuiadhirisha Simba SC kwa magoli 3-2 katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .

 

Azam FC walibadili imani ya mashabiki kwa kuonyesha kandanda safi katika vipindi vyite viwili huku wakiwaacha wachezaji wa Simba wakishindwa kuelewa cha kufanya.

 

Wakitumia mfumo mpya wa 4-3-3 upande wa Azam FC waliweza kufanya mchezo kuwa mgumu kwa Simba ambao wamezoea kutumia mfumo wa 4-4-2.

 

Simba SC walianza kupata goli dakika ya nane kupitia kwa mchezaji Nico Nyagawa, goli hilo lilidumu kwa dakika nne kabla ya mshambuliaji mahiri wa Azam FC John Bocco ‘Adebayo’ kusawazisha goli hilo katika dakika ya 13 kwa kichwa akiunga mpira wa Jamal Mnyate.

 

Goli hilo la kusawasazisha lilibadilisha hali ya mchezo, Azam FC waliongeza mashambulizi na dakika kumi baadaye MVP Mrisho Ngassa alimpoteza kipa wa Simba Juma Kaseja na kuandika goli la kuongoza katika dakika ya 23 kwa shuti liliingia moja kwa moja wavuni.

 

Hadi mapumziko Azam FC ilikuwa mbele kwa 2-1 dhidi ya mabingwa watetezi Simba SC , kipindi cha pili Simba walianza kufanya mabadiliko kwa kumtoa Nocco Nyagawa na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Ahmed ‘Shiboli.

 

Mabadiliko hayo hayakuzuia mashambulizi ya wachezaji wa Azam FC waliokuwa wakiongozwa na nahodha Ibrahim Shikanda, waliandika goli la tatu dakika ya 54 ya mchezo kupitia kwa John Bocco aliyetumia uzembe wa kipa Kaseja na kuachia shuti la mbali lililowaacha mabeki wa Simba Haruna Shamte na Meshack Abel na kuingia wavuni.

 

Baada ya goli hilo Azam FC walianza kucheza soka la burudani kwa kipindi chote huku wachezaji Salum aboubakar, Mrisho Ngassa, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Mutesa Mafisango walionekana mwiba wa Simba kwa kucheza zaidi ya pass sita.

 

Azam FC wakimtumia kwa mara ya kwanza kocha msaidi Kally Ongala aliyeanza kazi kwa baraka, walifanya mabadiliko walitoka Jamal Mnyate na John Bocco wakaingia Himid Mao na Peter Ssenyonjo ambao walizidi kuongeza maaumivu kwa kikosi hicho chenye maskani yake mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam .

 

Goli la pili la Simba lilifungwa dakika ya 87 na mchezaji Hilary Echesa, na kukamisha mchezo Azam FC ikitoka na pointi tatu muhimu na kufikisha  jumla ya pointi 23 huku Simba wakibaki katika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 27 wakati Yanga ikiongoza kwa pointi 28.

 

Kocha wa Azam FC muingereza Stewart Hall ameridhishwa na kiwango cha timu yake na kusema huo ni mwanza wachezaji wake wameanza kuuelewa mfumo wa 4-3-3 na kucheza kandanda safi .

 

Kikosi cha Azam FC kilichoibuka na ushindi, Vladimir Niyonkuru, Shikanda, Mafisango, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Mwaipopo, Mnyate/Himid Mao, Salum Aboubakar, Bocco/Senyonjo, Chombo na Ngassa