Mpira fitna na ujanja ujanja wa kupita milango ya nyuma leo vimeshindwa kufua dafu baada ya Azam FC kuipa kisago cha paka mwizi cha 3-2 Simba SC ambayo leo iligeuka paka na kuusaka mpira kwa tochi dakika 90 bila mafanikio.

Matunda ya kubalidilisha benchi la ufundi kwa Azam FC yameanza kuonekana leo baada ya Stewart Hall kufanya mabadiliko matano uwanjani

Stewart akishirikiana na Kally Ongala wamembadili Patrick Mafisango toka Holding Midfield na kumchezesha beki wa kushoto, halafu wakampanga Ibrahim Mwaipopo kama Holding  Midfielder.

Pia wamempeleka Mrisho Ngasa pembeni na kumuingiza Ramadhani Chombo Redondo ambaye Stewart anamuita Tevez eneo la kati kama msaidizi wa Bocco yaani namba kumi. Na badiliko la mwisho ni kumpeleka benchi Selemani Kassim Selembe na kumpanga kinda Jamal Mnyate.

Mabadiliko haya yameonesha kuwa makocha waliopo wanatoa nafasi kwa wachezaji walio katika hali nzuri na siyo kujuana kama ilivyo kwenye timu nyingi za Tanzania. Hii ni muhimu sana katika maendeleo ya timu na inajenga nidhamu na ueledi. Mtandao wa Azam FC unalipongeza benchi la ufundi la Azam FC.

Simba ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata goli mwanzoni kabisa mwa kipindi cha kwanza baada ya Nicco Nyagawa kupiga shuti lililombabatiza Mussa Hassan Mgosi na kutinga wavuni.

Baada ya goli hilo  vijana wa Azam FC walitulia na kuanza kucheza mpira wao wa gonga kama Barcelona kiasi cha kuwachanganya Simba SC ambao walikuwa hawajielewi na wengi wao walionekana kama wanadhani wanacheza na TP Mazembe na kabla hawajatulia vizuri Ibrahim Shikanda alipiga krosi safi iliyotua kichwani mwa Jamal Mnyate naye akampasia John Raphael Bocco kwenye Box ambaye alitulia na kupiga kichwa kilichotinga wavuni na kuandika goli la kusawazisha kwa upande wa Azam FC.

Wakati Simba SC wakidhani watasawazisha na kujitutumua kujaribu kupeleka mashambulizi mbele harakati zao zilishindwa kufurukuta kutokana na kuzidiwa mbinu na umilikaji mzuri wa mpira wa vijana wa Azam FC.

Azam FC waliendelea kumiliki mpira na kupiga pasi za uhakika zenye malengo toka nyuma hadi mbele huku wachezaji wake wakionekana kujiamini sana. Haya ni matunda ya mafunzo ambayo wanapata toka kwa kocha mkubwa mwenye mbinu na anayejua anachokifanya Stewart Hall.

Katikati ya kipindi cha kwanza Azam FC waliandika goli la pili baada ya Ramadhani Chombo Redondo kumpiga chenga Nyosso na kutoa pasi nzuri kwa Ngasa ambaye naye aliwazidi spidi walinzi wa Simba na kipa Juma Kaseja alipotoka naye alipigwa chenga na Ngassa kwenda far post ambako aliujaza mpira kwenye nyavu za Simba.

Hadi mapumziko azam 2-1 Simba SC

Kipindi cha pili kilipoanza Azam FC ilianza kwa kujiamini na kuendelea kumiliki mpira kiasi cha kushangiliwa na mashabili lukuki waliojanaza uwanjani. Simba SC walifanya mabadiliko kwa kumtoa Nicco Nyagawa na kumuingiza Shiboli Ally ili kujaribu kukabiliana na Azam FC lakini mabadiliko yao ndiyo yaliyowatesa zaidi kwani angala Nicco alikuwa akikaba kwa bidii na kupunguza pasi za Azam FC lakini Shiboli alipoingia Azam FC walijinafasi na kuzidisha mbwembwe kama Barcelona

Baadaye John Raphael Bocco aliifungia Azam FC goli la tatu baada ya kupokea pasi ya Himid mao ambaye aliingia badala ya Jamal Mnyate. Wakati Bocco anaukimbiza mpira golikipa Juma Kaseja alitoka na kumfanya Bocco kufunga kirahisi kwa kupiga cave iliyotinya wavuni.

Kilichotokeo baada ya hapo ilikuwa ni dharau kwa Azam FC kucheza pasi ambazo zilikuwa zikihesabiwa hadi 40 – 10 – 22 – 12 – 15 nk na Azam FC walikosa magoli mengi kupitia kwa Ngasa, SureBoy, Himid, Redondo na Bocco ambao kama waliridhika na ushindi wa 3-1

Baadaye wakati kila mtu akiamni kuwa mpira ungeisha kwa 3-1. Simba walipata goli la pili kwa shuti kali la mbali la Hilary Echessa

Azam FC iliwakilishwa na Vladmir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Patrick Mafisango, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Ibrahim Mwaipopo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, John Bocco/Peter SSenyenjo, Ramadhani Chombo na Jama Myate/Himid Mao

Simba SCiliwakilishwa na Juma Kaseja, Shamte Ally, Amir Maftah, Juma Nyoso, Meshak Abel, Jerry Santo, Niko Nyagawa/Mohammed Banka, Echesa Hilary, Mussa mgosi, Patrick Ochan Rashid Gumbo/Shiboli Ally