Mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara umeanza vibaya kwa timu ya Azam FC kwa kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar, katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

 

Azam FC ikiwa nyumbani imepoteza mchezo huo huku pia ikiwakosa wachezaji wake muhimu waliokatika timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inayoshiriki michuano ya Mto Nile nchini Misri.

 

Katika mchezo huo ambao Kagera Sugar imeshinda 2-1, kocha Azam FC wa Stewart Hall alianza kikosi chake kwa kumuweka mchezaji Samir Haji Nuhu katika kikosi cha kwanza ili kumpa uwezo wa kucheza katika mechi zijazo.

 

Mchezaji huyo chipukizi kutoka timu ya Azam Academy alionyesha uwezo wa hali ya juu kwa kucheza dakika zote 90 akiwa sambamba na walinzi wengine Ibrahim Shikanda, Mutesa Mafisango na Erasto Nyoni.

 

Pengo la wachezaji Agrey Moris na Mrisho Ngassa limeonekana wazi katika mchezo wa leo ambao umechezwa katika uwanja uliokarabatiwa wa Mkwakwani.

 

Akizungumza mchezo huo muda mchache baada ya kukamilika Kocha Stewart amesema mchezo ulikuwa mgumu na timu yake licha ya kumiliki mpira haikucheza katika kiwango kinachotakiwa.

 

“wachezaji wamecheza bila umakini, nashindwa kuwaelewa wanashindwa kucheza katika kiwango kizuri, wanapoteza mipira na kukosa nafasi nyingi za wazi.” kocha Stewart aliongea kwa masikitiko.

 

Katika mchezo wa leo mchezaji Gaudence Mwaikimba ameifungia Kagera Sugar magoli mawili, goli la kwanza dakika ya 3 na goli la pili lilifungwa kwa mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa Azam FC, Mutesa Mfisango kuunawa mpira katika eneo la hatari.

 

Goli la Azam FC limefungwa dakika ya 25 na mchezaji Ramadhani Chombo ‘Redondo’ aliyepiga mpira wa adhabu uliotinga moja kwa moja katika lango la Kagera Sugar.

 

Azam FC mchezo wa pili itacheza dhidi ya Simba SC katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .