Ni takribani miezi miwili na wiki moja imepita tangia raundi ya kwanza ya ligi kuu ya Vodacom imalizike na hivyo ligi kuu isimame. Azam FC ilimaliza raundi hiyo ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 20 baada ya kushinda michezo sita, kutoka sare michezo miwili na kufungwa michezo mitatu.

 

Azam FC itashuka kwenye dimba la Mkwakwani lililokarabariwa kuwakabili Kagera Sugar timu ambayo kwenye raundi ya kwanza kule bukoba iliifunga Azam FC 1-0. Kwa hiyo mechi ya kesho itakuwa ya kulipa kisasi.

 

Mchezaji nyota wa Azam FC John Bocco Adebayor hakuwa na msimu mzuri sana kwani baada ya kufunga magoli mawili kwenye mechi ya kwanza dhidi ya AFC hakuweza kuzifumania nyavu tena hadi raundi hiyo ilipofika kikomo.

 

Lakini wachezaji chipukizi wawili wa Azam FC Mau Boffu Ally na Salum Abubakar  SureBoy waling’ara vilivyo na walikuwa kwenye kikosi cha kwanza michezo yote ya Raundi ya kwanza.

 

Azam FC haikutarajia kumkosa kiungo wake Ibrahim Mwaipopo au kuporomoka kiwango kwa nahodha wake Salum Swedi ambaye sasa amerudi kwenye timu yake ya zamani ya Mtibwa Sugar.

 

Licha ya kutosajiri mchezaji yeyote, Azam FC imeongeza nguvu kwenye kikosi chake baada ya Ibrahim Mwaipopo kupona huku benchi la ufundi likiongozwa na Mwalimu wa waalimu mwenye elimu kubwa na utaalamu wa hali ya juu wa kufundisha Stewart John Hall.

 

Licha ya serekali kuruhusu kutumika uwanja mkuu wa taifa kwenye mechi za ligi kuu msimu huu. Azam FC imeamua kutumia uwanja wa mkwakwani kucheza mechi yake ya kwanza baada ya hapo kujua mustakbari wake wa kurejea jijini DSM.

 

Akizungumzia mechi ya kesho dhidi ya Kagera Sugar, kocha mkuu wa Azam FC Stewart Hall amesema, ana matumaini makubwa ya ushindi kwani timu yake imejiandaa vema na wachezaji wake wote muhimu wapo katika hali nzuri ya mchezo.

 

Azam FC ilitua Tanga juzi ikitokea jijini Dar es Salaam ambapo ilikuwa na maandalizi kabambe kujiandaa na ligi kuu.

 

Yote kwa yote tunasubiri hiyo kesho tuweze kujua kilichojiri huko Tanga. Tovuti hii ya Klabu na Facebook Page zitawaletea kilichojiri kwenye mechi hiyo.