Ni kama mazingaombwe lakini ndicho kinachotokea kwenye uwanja wa Amaan mjini Zanzibar ambapo timu kubwa zinaendelea kuadhirika mbele ya timu ambazo zilidhaniwa kuwa ni ndogo.

Walianza Yanga kutoka sare na Ocean View ya Zanzibar na Simba waliwacheka sana Yanga lakini ilipofika zamu yao dhidi ya Jamhuri ya Pemba Simba nao walijikuta wakikaliwa kooni na kwenda sare na Jamhuri ya Pemba.

Leo mchana kama siyo utaalamu wa kocha Stewart Hall ambaye alilazimika kubadili mbinu na wachezaji kuweza kusawazisha na kupata sare ya 2-2, Azam FC ingeweza kulala 2-0 mbele ya mabingwa wa Zanzibar Ocean View.

Lakini Burudani ilikuwa jioni baada ya Yanga kushindwa tena kufurukuta na kwenda sare ya 0-0 na Chuoni timu iliyopokea kisago cha 3-0 toka kwa Azam FC kwenye mechi ya ufunguzi.

Sasa kila mtu ameelewa somo kuwa mapindizi Cup 2011 siyo masihara na timu zote zinazoshiriki zimejiandaa vema.

Katika mchezo wa leo, kosa la walinzi wa Azam FC Mutesa Mafisango na Erasto Nyoni kugongana na kutoa pasi fupi kwa kipa kulimpa nafasi kiungo mkongwe na nahodha wa Ocean View Sabri Ramadhani China kufunga goli la awali kwa timu yake.

Azam wakidhani wangesawazisha walijikuta wakipachikwa goli la pili katika dakika ya 55 ndipo kocha Stewart Hall alipomtoa Salum Abubakar na kumuingiza Tumba Swedi kwenda kuchukua nafasi ya Mutesa Mafisango ambaye alisogezwa mbele na mabadiliko hayo yaliipa Azam FC goli la kwanza kupitia kwa John Raphael Bocco aliyefunga kwa kichwa.

Baadaye kidogo kinda mwenye kasi na mashuti makali Jamal Mnyate aliipatia Azam FC goli la kusawazisha kwa shuti kali baada ya kuwazidi maarifa na nguvu walinzi wa Ocean View na kuachia kombola lililotinga wavuni moja kwa moja

Mechi nyingine zitaendelea kesho kwa Simba kucheza na KMKM na Jamhuri kucheza na Mtibwa Sugar