Wenzetu katika nchi zilizoendelea wanathamini sana rekodi, kwenye klabu kubwa wachezaji na makocha wanajaribu sana kujenga rekodi zao binafsi kama kucheza mechi nyingi bila kupoteza, kucheza mechi nyingi zaidi, kutokuruhusu wavu wao kutikiswa na kadhalika.

Katibu mkuu wetu Nassor Idrissa ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa katibu mkuu wa kwanza wa kuajiliwa kwa vilabu na jina lake kuwasilishwa TFF. Upande wa wachezaji mchezaji wetu John Bocco ndiye anayeshikiria rekodi ya kuifungia Azam FC magoli mengi hadi sasa huku kipa Vladmir Niyonkuru akiwa ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi mfululizo lakini rekodi ya wingi wa mechi kwa ujumla inashikiliwa na kiungo Salum Abubakar. Ipo siku tutaandaa taarifa rasmi ya nani kafanya nini ndani ya klabu

Leo katika uwanja wa Amaan Azam FC imefikisha usindi wa saba mfululizo ushindia ambao umeweka rekodi kwa timu kushinda mechi nyingi mfululizo.

Azam FC iliifunga Polisi Dodoma 0-1, baada ya hapo ikaifunga Ruvu Shooting 4-1, hii ilikuwa kwenye mechi mbili za mwisho wa mzunguko wa kwanza ligi kuu.

Baada ya hapo Azam FC ikacheza na Simba SC na kuifunga 3-2, ikakumbana na Yanga na kuisasambua 3-1, ikacheza na African Lyon na kuibanjua 2-1 kabla ya kupeleka kisago cha mbwa mwizi kwa AFC Leopards ya Kenya cha 4-0 na leo imeifunga Chouni 3-0 na kufikisha rekodi ya kipekee ya 7-0-0 yaani kushnda mechi saba, kutoka sare sifuri na kufungwa sifuri.

 

Magoli ya leo yamefungwa na Seleman Kassim ‘Selembe’, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Ibrahim Mwaipopo.

 

Mashindano hayo maalumu yanayofanyika kila mwaka ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mapinduzi ambayo huwa Januari 12, mashindano hayo hujumuisha timu nne kutoka Tanzania bara na timu nne kutoka Zanzibar .

 

Azam FC iliyotawala mchezo nyakati zote, ilipata goli la kwanza dakika ya 25 kupitia kwa  mchezaji Seleman Kassim Selembe aliyepokea pass nzuri kutoka kwa John Bocco.

 

Goli hilo lilidumu hadi mapumziko, muda wote wa mchezo Azam FC walimiliki mpira na kutoa nafasi chache kwa timu ya Chuoni ambayo imepanda daraja msimu huu.

 

Chuoni walijitahidi kuleta upinzani katika mchezo huo lakini haikuweza kufurukuta mbele ya vijana wa Azam FC. kipindi cha pili Azam FC walifanya mabadiliko ya kwanza dakika ya 45 alitoka John Bocco na nafasi yake kuchukuliwa vyema na Peter Ssenyonjo.

 

Mabadiliko hayo yalileta matunda kwa Azam FC, dk ya 54 Ramadhani Chombo ‘Redondo’ aliandika goli la pili kwa kucheza vizuri pass ya Ssenyonjo ambapo aina ya shambulizi lilikuwa kama pacha na lile la goli la kwanza.

 

Azam FC walibadilika na kuwa kama ndio wanaanza mchezo, walicheza mpira mzuri unaoonekana licha ya Chuoni kufanya mabadiliko mara mbili mfululizo kwa kuwatoa Ally Mngazija na Seleman Ally ambao nafasi zao zilichukuliwa na Ally Salum na Omary Makungu.

 

Chuoni wakifanya mabadiliko hayo Azam FC iliwatoa, Kally Ongala, Selemani Kassim na Mau Bofu nafasi zao kuchukuliwa na Jamal Mnyate, Himid Mao na Tumba Swed.

 

Mabadiliko hayo yaliongeza nguvu kwa Azam FC, dakika ya 81 kiungo Ibrahim Mwaipopo alikamilisha karamu ya magoli akiachia shuti lililotinga moja kwa moja wavuni baada ya kuwachambua mabeki wa Chuoni.

 

Azam FC, Vladimir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Mau Bofu/Tumba Swed, Mutesa Mafisango, Ibrahim Mwaipopo, Seleman/Himid Mao, Bocco/Ssenyonjo, Salum Aboubakar, Kally/ Jamal Mnyate. Chombo.