Uongozi wa Azam FC umethibitisha kuingia mkataba na kocha Stewart Hall wa Zanzibar Heroes kuchukua nafasi ya kuifundisha timu hiyo baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Itamar Amorin.

 

Azam FC imemchukua kocha huyo baada ya kuridhishwa na CV yake, rekodi yake kama kocha na pia utendaji kazi aliouonesha kwa kipindi kifupi alichoanza kuifundisha timu hiyo ya taifa ya Zanzibar.

 

Katibu Mkuu wa klabu hiyo Nassor Idrissa amesema wameangalia vyeti vyake na ujuzi alionao hivyo wakaamua kumpa nafasi hiyo.

 

Lakini katibu mkuu Nassor Idrissa akasisitiza kuwa Stewart hakuwa mmoja kati ya makocha waliokuwa wakiwahitaji lakini jina lake lilikuja ghafla wakati mashindano ya CECAFA yakiendelea baada ya kucha huyo mwenyewe kuwasilisha CV yake na kuuambia uongozi wa Azam FC kuwa baada ya CECAFA atakuwa kama hana kazi kutokana na Zanzibar kutoshiriki mashindano yoyote hivyo kupoteza fedha za wafadhili wake.

 

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyowekwa kati ya Azam FC na kocha Stewart, Stewart ataendelea kuwa Mshauri wa ufundi wa ZFA bure na ataendelea kuisaidia Zanzibar kama sehemu ya benchi la ufundi hadi pale Zanzibar itakapopata kocha mwingine kuchukua nafasi yake.

 

“Uteuzi wa kocha sio kitu rahisi kama watu wanavyofikiria, tumechukua muda wote huo kuangalia wasifu wa makaocha wote walioleta maombi yao na kufikia kumchagua kocha Stewart John Hall ambaye tumeshuhudia uwezo wake akiwa na Zanzibar Heroes.”amesema Nassor.

 

Nassor amesema kocha huyo atawekwa hadharani muda wowote kuanzia leo baada ya kukamilika kwa taratibu za kiofisi na ataanza kazi mapema iwezekanavyo, ili kuanza maandalizi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu utakaoanza mapema mwezi January mwaka kesho.

 

Kocha huyo raia wa Uingereza ni mkufunzi wa makocha nchini Uingereza pia ana leseni ya juu ya ukocha kutoka shirikisho la mpira wa miguu barani Ulaya UEFA (UEFA Professional Licence), akiwa amefundisha timu za wakubwa, vijana na watoto (grassroots).

 

Baadhi ya timu alizofundisha Stewart ni Halesowen Town FC iliyopo kusini mwa Uingereza, San Juan Jablotei ya Tridad and Tobago, kocha wa msaidizi wa Brimingham City mwaka 2003-4, Pune FC ya India mwaka 2008-9, St Vincent &The Grenadines kocha mkuu mwaka 2010.

 

Baadhi ya Makocha aliowafundisha na kufanyanao kazi ni pamoja na John Peacock wa ligi Uingereza, Dick Bate, Roy Miller mkurugenzi wa makocha Ireland ya Kaskazini, Steve Bruce wa Sunderland na Gareth Southgate aliyekuwa kocha wa Middlesbrought FC.