Kazi nzuri ya wachezaji chipukizi wa Azam FC imewapatia ushindi wa 3-2 dhidi ya timu ya Simba SC katika mechi ya kirafiki ya tamasha la AMKA Kijana iliyochezwa leo katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC katika mechi hiyo walidhihirisha umahiri wa wachezaji wake chipukizi waliochukua vyema nafasi za wachezaji tisa wa timu hiyo wanaliopo katika timu zao za taifa.

 

Kipindi cha kwanza timu zote zilianza kwa kusomana kwani dakika ya nane mchezaji Fredy Cosmas alianza kwa kujaribu lakini mpira ulitoka nje mita chache karibu na goli Simba.

 

Uwezo mkubwa wa kiungo Ibrahim Mwaipopo uliweza kulete burudani na kuhimiza timu kufanya vizuri lakini dakika ya 36 Simba waliandika goli la kwanza kipitia kwa mchezaji Kelvin Chale.

 

Dakika nne baadaye mshambuliaji mwenye uwezo wa kuachia mashuti ya umbali wowote Ally Manzi aliweza kuandika goli la kusawazisha kwa kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango Kabali Faraji wa Simba SC.

 

Baada ya Azam FC kusawazisha goli hilo mpira ulibadilika na kuwa wa kushambuliana mara kwa mara huku wachezaji Ramadhan Chombo 'Redondo' na Kali Ongala wakiweza kumiliki mpira vizuri nyakati zote na kuacha wachezaji wa Simba SC kupotezana, hadi mapumziko timu zilitoka 1-1.

 

Kipindi cha pili Azam FC walikuja na kasi mpya ya kutafuta ushindi kwani dakika ya 49 Fredy Cosmas aliweza kufunga goli la pili baada ya kutumia vyema uzembe wa mabeki wa Simba kwa kupenya katikati yao na kuachia mpira ulioenda moja kwa moja katika lango la Simba.

 

Goli hilo lilizidi kuamsha kasi ya mchezo, Simba wakitaka kurudisha Azam FC walihitaji kuongeza lingine, hali hiyo ilipelekea kuchezwa kwa mpira wa kiwango cha juu kwa muda wadakika kumi, Mau Bofu, Tumba, Aboubakar Salum 'Sure Boy' wakisumbua kikosi cha Simba mara kwa mara.

 

Simba walisawazisha goli hilo dakika ya 59 kupitia kwa mchezaji wao Rashid Gumbo aliyepokea pasi ya Salum Kanoni. Goli hilo halikuweza kukaa muda mrefu kwani Azam FC walifanya mabadiliko kwa kuwarudisha benchi Kali Ongala, Ally Manzi na Malika Ndeule huku nafasi zao zikichukuliwa vyema na vijana Jukum Kibanda, Ahmed Mkweche, Simon Msufa na Omary Mtaki.

 

Mabadiliko hayo yaliweza kuleta mafanikio kwani dakika ya 68 Simon Msufa akiwa amevalia jezi namba tano aliweza kuandika goli la kuongoza kwa mpira wa kichwa akiwa amepokea pasi kutoka kwa Aboubakar Salum 'Sure Boy' aliyecheza vizuri mpira wa Mwaipopo.

 

Mwaipopo akiwa mchezaji wa mechi sambamba na Tumba, Redondo na Fred aliweza vyema kuokoa mpira ya Simba na kuzidisha mashambulizi kwani dakika tano kabla ya mchezo kumalizika Azam FC walitoa mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba lakini hayakuweza kubadilisha matokeo hayo.

 

Hivyo Azam FC wakaondoka na ushindi huo wakiwa chini ya makocha wawili katika benchi lao Habib Kondo na Herry Mzozo.

 

Azam FC: David Gabriel, Ibrahim Mwaipopo, Malika Ndeule/Ahmed Mkweche, Kally Ongala/Omary Mtaki, Ramadhan Chombo Redondo, Ally Manzi/Simon Msufa, Himid Mao/ Jukumu Kibanda, Mau Bofu, Aboubakar Salum 'Sure', Fredy Cosmas na Tumba Swed.