Baada ya kumaliza mkataba wake wa kuitumikia Azam FC, nahodha wetu Salum Swed atapumzika ili kutoa nafasi kwa kijana mwingine kupanda kwenye kikosi cha kwanza na sasa, Klabu ya Azam FC inataraji kumpandisha beki anayechipukia Tumba Swed kutoka Azam Academy kwenda Azam FC kuchukua nafasi ya kaka yake Salum Swed.

 

Taarifa kutoka kwa katibu mkuu Nassor Idrissa  zimeiambia tovuti ya www.azamfc.co.tz kuwa Salum Swed amemaliza mkataba wake na kutokana na maendeleo ya Tumba imebidi nafasi yake ichukuliwe na kinda huyu mrefu mwenye uwezo mkubwa sana ambaye amethibitisha ubora wake tangu akiwa kwenye academy.

 

“Salum Swedi amemaliza mkataba wake mwezi huu, ameichezea Azam FC kwa mafanikio makubwa na nidhamu ya hali ya juu sana. Azam FC itaendelea kumkumbuka nahodha huyu kutokana na utiifu, nidhamu, bidii mazoezini na kiwanjani, Kwa msimu ujao hatutakuwa nae tena na nafasi yake tunataraji kumpatia Tumba Swed kutoka timu yetu ya Academy.” amesema Nassor Idrissa, Katibu Mkuu wa Azam FC.

 

Amesema kuhusu usajili bado hawajafikia makubaliano kusajili mcheza mpya yoyote zaidi kuwapandisha wachezaji wa timu ndogo, kwani nafasi ya wachezaji wa kimataifa imeshajaa imebaki nafasi chache za wachezaji wa ndani.