Magoli matatu ya mchezaji Mrisho Ngassa yameweza kuipatia ushindi timu ya Azam FC wa magoli 4-1 dhidi ya Ruvu Shooting na kuifikisha nafasi ya tatu na kuifanya kwenda mapumziko baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa katika nafasi hiyo.

 

Kwa matokeo hayo, Azam FC imeitoa Mtibwa Sugar katika nafasi hiyo kwa kuwa na pointi 20 ikifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye pointi 19.

 

Azam FC imeweza kufikia nafasi hiyo kwa kuonyesha kandanda safi katika kipindi cha pili, uwezo wa wachezaji Jamal Mnyate na Peter Senyonjo waliochukua nafasi za  John Bocco na Jabir Aziz umeweza kuleta idadi hiyo ya magoli kwani hadi timu zinakwenda mapumziko Ruvu Shooting walikuwa mbele kwa 1-0 lililofungwa dakika ya 35 na mshambuliaji Paul Ndauka.

 

Kipindi cha pili Azam FC walianza kwa kutoa shambulio la kwanza katika dakika ya 47 ambako mchezaji John Bocco aliruka juu sambamba na beki wa Ruvu kuuwahi mpira ambao ulianguka na kutua miguu kwa Ngassa na kuweza kusawazisha goli hilo.

 

Wakitaka kumaliza vyema katika uwanja wao wa nyumbani Azam FC waliendeleza mashambulizi na dakika ya 74 nyota wa mchezo huo Ngassa aliweza kuandika goli la pili kwa mkwaju wa penalt baada ya mchezaji Ndauka kuunawa mpira katika eneo la hatari, na mwamuzi wa mchezo huo Daudi Paul kutoka Mtwara akampa kadi ya njano.

 

Dakika sita baadaye mshambuliaji kutoka Uganda, Peter Senyonjo aliweza kuipatia Azam FC goli la tatu baada ya kuonana vizuri sana na Mnyate ambaye alimtupia pande kutoka upande wa kushoto na kuuingiza moja kwa moja katika nyavu za Ruvu Shooting.

 

Wakiwa bado wakistaajabu kipigo cha magoli matatu, Ruvu Shooting walijikuta wakifungwa goli la tatu na Mrisho Ngassa ambaye aliweza kuachia shuti kati la mbali lililotua moja kwa moja nyavuni na kuinua shangwe kwa mashabiki wa Azam FC huku akiacha midomo wazi kwa Ruvu Shooting ambao walijua mpira ule hautafika golini.

 

Wachezaji walioweza kunga’ara katika mchezo wa leo ni Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mutesa Mafisango, Mau Ally, Shikanda  na golikipa Vladimir Niyonkuru.

 

Kikosi kilichomaliza mzunguko huo ni Vladimir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Mau Bofu, Aggrey Morice, Salum Swed, Mutesa Mafisango, Jabir Aziz/Jamal Mnyate, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, John Bocco/Peter Senyonjo, Ngassa na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.