Uongozi wa Klabu ya Azam FC umesitisha mkataba wa Kocha Mkuu wa klabu hiyo Itamar Amourim katika kile kinachoitwa (Makubaliano ya pande zote mbili ) lengo likiwa ni kulinda maslahi ya klabu na kocha mwenyewe.

 

Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa amesema wamefikia hatua hiyo ili kuleta maendeleo zaidi katika klabu hiyo pia na kulinda heshma ya kocha huyo.

 

“Tumekaa, tukajadili maendeleo ya timu na kufikia uamuzi huo, tumekubaliana kusitisha mkataba wa Itamar kwa lengo la kuleta maendeleo katika klabu, hatuja mfukuza, tumekatisha mkataba kirafiki” amesema Idrissa.

 

Ameongeza kuwa timu iko katika nafasi nzuri ya ligi, hivyo ni makubaliano yaliyofikia maamuzi hayo hayatokani na kigezo cha kufanya vibaya kwa timu.

 

Nassor amesema wanatambua umuhimu wa kocha huyo, wanamshukuru kwa mchango wake alioutoa tangu alipojiunga na timu hiyo.

 

Mkataba wa kocha Itamar ulitakiwa kukamilika mwisho wa msimu huu wa 2010/2011, kocha huyo anaicha timu ikiwa katika nafasi ya 4, katika msimamo wa ligi ikiwa imepoteza michezo mitatu, imetoka sare michezo miwili na kushinda michezo mitano, Azam imebakisha mchezo mmoja kukamisha mzunguko wa kwanza.

 

Akizungumzia wa kukaimu nafasi yake kwa sasa, Nassor amesema wapo kitika mazungumzo hivyo wa kuchukua nafasi yake atatangazwa muda si mrefu.

 

Kocha Itamar alijunga kuifundisha timu hiyo katika msimu wa 2008/09 akiwa kocha msaidizi chini ya kocha Neider Dos Santos, alishika nafasi ya kuwa kocha mkuu na mkurugenzi wa ufundi wa Azam FC mwishoni mwa msimu wa ligi kuu 2008/9

 

Alifanikiwa kuiokoa Azam FC na janga la kushuka daraja 2008/9 kabla ya kuipa mafanikio timu hiyo kwa kumaliza mshindi wa tatu katika msimu wa ligi uliopita wa 2009/10.