Goli la kichwa la nyota wa kimataifa toka Uganda Peter Ssenyonjo la dakika ya kumi ya mchezo limetosha kuipa Azam FC ushindi wa 1-0 katika mchezo mkali wa ligi kuu ya Vodacom  uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Kikosi cha Azam FC jioni ya  leo kilifanyiwa mabadiliko ya kiufundi tofauti na michezo mitatu iliyopita ambapo Jabir Aziz alianza kwenye dimba la kati mbele akimpokea Salum Abubakar,  Kalimangonga Ongala naye alianza pembeni badala ya Selemani Kassim Selembe na Peter Ssenyonjo akimbadili nyota  Mrisho Ngasa ambaye alipumzika jioni hii.

Mabadiliko hayo ambayo kocha Itamar Amorim aliyafanya yalikuwa na msaada mkubwa kwa timu kwani Ssenyonjo alionesha kiwango cha hali ya juu na kumfanya Bocco kung’ara jioni hii, Bocco licha ya kutofunga, lakini alikuwa hatari muda wote wa mchezo na mashuti yake matatu aliyoyapiga yaligonga mwamba wa goli la Polisi.

Erasto Nyoni ameendelea kuthibitisha thamani yake na bila shaka hivi sasa anaelekea kuwa beki bora wa kati nchini, nguvu zake zikichanganywa na uchezaji wake wa Jihad, uwezo wake wa kumiliki mpira ukichanganywa na akili nyingi anazotumia kukaba zinamfanya Erasto awe wa kipekee na kwa sasa, anakuwa mchezaji ambaye kila shabiki wa Azam FC anapenda kumuona uwanjani.

 

Ramadhani Chombo Redondo anaendelea kuwa mchezaji wa kipekee, Redondo ambaye umaarufu wake unatokana na vitu adimu na vya kipekee alivyonavyo mguuni, leo aliwapa shida sana wachezaji wa polisi kumkaba na kumfanya aendelee kuufurahia mchezo wa mpira na kufurahisha mashabiki wake,

Mchezaji mwingine ambaye tusipomzungumzia tutakuwa tumemnyima halki yake ni Mutesa Mafisango Patrick, Nyota huyu na nahodha wa zamani wa APR na timu ya Taifa ya Rwanda leo amecheza kwa kiwango cha juu na kukonga nyoyo za mashabiki waliojazana kwenye uwanja wa Jamhuri.

Jambo moja la kufurahia leo hii na katika mechi zote ambazo Azam FC wanacheza ni jinsi mashabiki wanavyojazana kiwanjani, leo jukwaa kuu lilitapika mashabiki na uchunguzi wa tovuti ya Azam FC umeonesha kuwa, ni mechi hii na ile ya Yanga ndizo zilizojawa mashabiki kwenye uwanja huo, hali hiyo pia ilijionesha Songea ambako baadhi ya mashabiki walikuwa na hamu ya kuwaona akina ngasa na wengine kwenda kuwakumbatia.

Manungu pia ilijaa kama ilivyokuwa Mwanza, kagera na tanga ambapo Azam FC inacheza, hii inamaanisha kuwa Azam FC ya mwaka huu ni tofauti na mwaka jana na inaonesha kuwa timu hii imekuwa ikikua kila kukicha.

Katika mchezo wa leo wachezaji wawili wa Polisi Tanzania walipewa kadi Nyekundu wa kwanza alikuwa beki wa kimataifa wa Tanzania na Zanzibar Salmin kisu kwa kuzozana na Mwamuzi katika dakika ya 70  na wa pili alikuwa ni beki mwingine wa kati ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kwenye dakika 90. 

Azam FC; 

1. Vladmir Niyonkuru
2. Ibrahim Shikanda (El Kapitano)
3. Mau Boffu Ally
4. Aggrey Morris Chacha
5. Erasto Nyoni Mashine
6. Patrick Mutesa Mafisango
7. Kalimangonga Ongala/Fara Husein
8. Jabir Aziz
9. John Bocco Adebayor/Mrisho Ngasa
10. Peter Ssenyonjo
11. Ramadhani Chombo