Timu ya Azam FC jana jioni ililazimishwa sare ya bila kufungana na timu ya Yanga katika mchezo mkali uliochezwa kwenye uwanja wa mkwakwani mkoani Tanga.

 

Azam FC wakiwa na kikosi kamili waliihenyesha Yanga muda wote wa mchezo kiasi cha kuvifanya vikundi vya kushangilia vya Vuvuzela na Yanga Bomba kuwa kimya muda wote wa mchezo.

 

Kutokana na matokeo hayo Azam FC imefikisha jumla ya pointi 14, huku Yanga ikiachia usukani kwa Simba baada ya kuwa na jumla ya pointi 21 sawa na Simba wakitofautiana katika magoli ya kufunga.

 

Katika mchezo wa jana, timu zote zilicheza kwa kukamiana, lakini ilikuwa ni Azam FC iliyoonekana kuwa na ufundi zaidi.

 

Katika kipindi cha kwanza, Azam FC walikuwa moto mkali kwani gonga zao na kasi ya wachezaji kama Ramadhani Chombo, Salum Abubakar na Mrisho Ngasa walishindwa kabisa kudhibitiwa na wachezaji wa Yanga ingawa mara kadhaa ubovu wa Uwanja na uchezeshaji mbovu wa mwamuzi uliathiri mipango ya Azam FC, hadi kufikia mapumziko Azam walikuwa wakiongoza kwa kuwa na kona sita huku Yanga wakiwa na jumla ya kona nne.

 

Mchezaji Mrisho Ngassa aliwadhihirihishia mashabiki wa Yanga kuwa sasa yupo Azam FC na si yanga tena, kwani mashuti na makeke yake pekee yaliweza kuzaaa kona tatu na faulo moja.

 

Mchezaji anayechipukia Mau Bofu aliweza kucheza mpira kwa kiwango cha juu na kumfanya mchezaji mkongwe, Godfrey Bonny wa Yanga kulazimika kumchezea vibaya mchezaji huyo na kupelekea kupewa kadi ya njano katika dakika ya 13.

 

Hadi kufika mapumziko matokeo yalikuwa 0-0, kipindi cha pili timu zote zilikuja kwa kasi, lakini ilikuwa ni Yanga iliyofanikiwa kujaribu uwezo wa kipa wa Azam FC Vladmir Niyonkuru ambaye aliweza kuzuia mashuti yaliyopigwa na wachezaji wa Yanga.

 

Mchezaji Nsa Job alikuwa na nia ya kuifunga timu yake ya zamani Azam FC lakini beki mahiri Erasto Nyoni aliweza kumdhibiti nyakati zote na kumfanya Nyota huyo wa Yanga kutoka kapa.

 

Timu zote zilifanya mabadiliko katika nyakati tofauti, mabadiliko ambayo yalileta mabadiliko ya mchezo, Yanga waliwatoa Nurdin Bakari, Jerryson Tegete na Abdi Kassim na nafasi zao kuchukuliwa na Omega Seme, Idd Mbaga na  Yahya Tumbo.

 

Azam FC walifanya mabadiliko kwa kuingia Ibrahim Mwaipopo, Jamal Mnyate na Peter Senyonjo ambao waliweza kuchukua vyema nafasi za Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Seleman Kassim ‘Selembe’ na John Bocco.

 

Kwa kiasi kikubwa Mabadiliko yaliyofanywa na Azam FC hayakuisaidia Azam FC hasa kutokana na kutoka kwa Salum Abubakar na kuingia Mwaipopo, Salum alikuwa na kasi na alikuwa akizunguka sana eneo la katikati na kuwafanya viungo wa yanga kushindwa kucheza, kutoka kwake kulwapa nafasi viungo wa Yanga na katika muda wate wakati Salum yupo nje Yanga walibadilika na kutawala eneo la kiungo

 

Dakika ya 81, Mwaipopo alikosa nafasi ya wazi baada ya kupiga mpira wa adhabu uliotoka nje, huku dakika ya 82, Iddi Mbaga naye alikosa goli kwa kupiga mpira uliotoka nje.

 

 

Azam FC, Vladimir, Shikanda, Mau Ally, Aggrey Moris, Erasto Nyoni, Mutesa Mafisango, Seleman Kassim ‘Selembe’/Jamal Mnyate, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’/Ibrahim Mwaipopo, John Bocco/Peter Senyonjo, Mrisho Ngassa, Ramdhan Chombo ‘Redondo’.