Lilikuwa suala la wakati tuu ndivyo ambavyo tunaweza kusema kwani baada ya kujikongoja kichovu kwenye mechi za awali, hatimaye Azam FC sasa imefunguka, MVP Mrisho Ngasa kafunguka na kila mmoja wetu anafurahia nafasi aliyonayo klabuni baada ya vijana leo tena kutoa Dozi kwa wakatamiwa wa Mtibwa Sugar kwa kuitandika 4-0.

Tangia kuanza kwa ligi kuu msimu huu hakuna timu iliyofunga zaidi ya magoli matatu, tena ni timu mbili tuu za Simba na AFC zilizofanikiwa kufikisha idadi hiyo ya magoli lakini Azam FC leo imetoa dozi ugenini Manungu Complex kwa timu ngumu na bora kabisa ya Mtibwa Sugar.

Ramadhani Chombo Redondo ndiye aliyefungua kitabu cha magoli baada ya kupokea pasi ya Salum Abubakar na kupiga mpira golini mwa Mtibwa ambapo Patrick Mafisango aliukwepa kiufundi na kumzubaisha kipa wa Mtibwa na timu ya Taifa Shaabani Kado.

Dakika moja kabla ya mapumziko, Kado alishindwa kuokoa mpira golini mwake na katika piga nikupige mpira ukafika miguuni mwa Golden Boy Mrisho Ngasa ambaye bila ajizi aliukwamisha kimiani na kufanya matokeo kuwa 2-0 wakati wa mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Mtibwa Sugar wakijaribu kusawazisha lakini ubora wa nyasi za kiwanja uliwapa nafasi zaidi Azam FC ambapo Azam FC waliendelea kutawala mchezo huku pasi zao zikiwafanya mamia wa mashabiki waliofurika Manungu Complex kushindwa kujizuia na kuamua kuishangilia Azam FC.

Karamu ya magoli iliendelea dakika ya 50 baada ya Ngasa tena kuukwamisha mpira kimiani kwa shuti kali baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa kati wa Mtibwa Sugar waliokuwa wakiongozwa na Salvatory Ntebe.

 

Baada ya goli hilo Azam FC iliamua kuwapumzisha Mrisho Ngasa ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Jamal Myate, Erasto Nyoni ambaye alimpisha Tumba Swedi na Selemani Kassim Selembe ambaye alimpisha Ibrahim Mwaipopo.

 

Mchezaji aliyeingia kutoka benchi Myate Jamal alikuwa na siku nzuri sana kwani kila mpira alioupata ulileta sokomoko kwenye lango la Mtibwa Sugar.

Baadaye katika dakika ya 62 juhudi za Mnyate zilizaa matunda baada ya kuwatoka walinzi wa Mtibwa kwa kasi na kuachia shuti kali lililotinga wavuni na kuiandikia timu yake ya Azam FC ushindi wa 4-0

Azam FC; Vladmir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Maulid Boffu Ally, Aggrey Morris, Erasto Nyoni/Tumba Swedi, Patrick Mafisango, Selemani Kassim Selembe/Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar, John Bocco, Mrisho Ngasa/Jamal Mnyate na Ramadhani Chombo Redondo.