Goli pekee la mshambuliaji ghali kuliko wote Tanzania ‘MVP’ Mrisho Ngassa limeipatia pointi tatu timu yake ya Azam FC katika mchezo wa Ligi kuu dhidi ya timu ya Majimaji wanalizombe uliochezwa katika uwanja wa Majimaji, mkoani Ruvuma.

 

Ngassa alianza kutafuta goli hilo toka kipindi cha kwanza lakini alikosa nafasi za wazi ambazo zilisababisha timu hiyo kupata kona nne katika kipindi cha kwanza.

 

Jitihada zake zilizaa matunda katika dakika ya 56 kipindi cha pili baada ya kuwaacha mabeki watatu wa Majimaji, Evarist Maganga, Lulanga Mapunda na Shabik Issa na kukokota mpira mita chache kabla ya kuingia eneo la penalt hadi kumkaribia goli kipa Majimaji Said Mohamed ambaye alishindwa kudhibiti shuti la Ngassa ambalo lilimpita upande wa kulia na kutinga nyavuni.

 

Katika mchezo huo Azam FC walionekana kubadilika na kucheza katika kiwango cha hali ya juu tofauti na michezo iliyopita. Katika kipindi cha kwanza Azam FC walionesha nia ya kutafuta ushindi katika mechi hiyo, walianza kwa kutoa shambulio la kwanza dakika ya tatu baada ya Ngassa kupata nafasi lakini golikipa Said Mohamed aliweza kuokoa mpira huo.

 

Vijana wa Azam FC hawakukata tamaa wachezaji John Bocco, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Mutesa Mafisango ambao walicheza kwa kiwango cha juu sana leo waliweza kupata nafasi ambazo zilizidi kuwapa wakati mgumu wachezaji wa Majimaji FC. Upande wa Majimaji walikuwa wakilinda sana lango lao na walipata nafasi chache ya kufanya mashambulizi. Shambulizi lao kubwa lilikuwa dakika ya 12 mchezaji Juma Mpola alipiga Shuli lililogonga mwamba na kutoka nje.

 

Hadi kufikia mapumziko timu zote zilikuwa suluhu huku Azam FC wakiutawala mchezo kwa asilimia kubwa, Azam FC walimaliza kipindi hicho wakiwa na kona nne na mipira ya adhabu mitatu huku Majimaji wakiwa na kona mbili na mpira wa adhabu mmoja.

 

Kipindi cha pili kilipoanza dakika 47 Azam FC walianza tena makeke yao baada ya mchezaji Chombo Ramadhan kuachia shuti liliingia mikononi mwa golikipa wa Majimajim Said Mohamed ambaye tunaweza kusema alikuwa nyota wa mchezo kwa upande wa Majimaji.

Dakika ya 50 beki wa katikati Erasto Nyoni alijaribu kulitia msokosuko lango la Majimaji baada ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi lakini shuti lake alilopiga ilitoka nje kidogo ya lango la Majimaji FC.

 

Dakika ya 55 Selemani Kassim alijaribu kuunganisha kona ya mchezaji Patrick Mafisango lakini iliokolewa na mabeki wa Majimaji ambao dakika ya 56 walishindwa kumdhibiti Ngassa aliyefunga goli pekee katika mchezo huo.

 

Goli hilo lililoifikishia Azam FC pointi 10, liliwaamsha Majimaji ambao waliaza kufanya mabadiliko katika dakika ya 64 kwa kutoka Peter Mapunda akaingia Hamis Adini na dakika ya 68 akaingia Said Ngappa na kutoka Shabil Issa lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuzuia mashambulizi ya Azam FC.

 

Azam FC wakitafuta goli la pili Chombo alikosa nafasi mbili za wazi katika dakika ya 82 na 83, huku Majimaji wakiwa katika hali ya kusawazisha goli hilo dakika ya 85 lakini mchezaji Kulwa Mobby alikosa nafasi ya wazi akiwa yeye na kipa wa Azam Jackson Chove na kuutoa mpira nje.

 

Azam FC walifanya mabadiliko dakika ya 68 alitoka Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ akaingia Jabir Aziz, na katika dakika ya 77 aliingia Peter Ssenyonjo kuchukua nafasi ya  John Bocco huku dakika ya 89 aliingia  Kally Ongala akitoka  Seleman Kassim ‘Selembe’.

 

Hadi kukamilika kwa mchezo huo Azam FC walimaliza wakiwa na jumla ya kona 12, mipira ya adhabu minne wakati Majimaji waliweza kupata kona 8 na mipira ya adhabu miwili.

 

Mwamuzi wa mchezo huo Zacharia Jacob aliweza kutafsiri sharia zote 17 za mpira wa miguu kwani hakukuwa na malalamiko yoyote.

 

 Azam FC, Jackson Chove, Ibrahim Shikanda, Mau Ally, Aggrey Morice, Erasto Nyoni, Mutesa Mafisango, Seleman Kassim/Kally Ongala, Salum Aboubakar/Jabir Aziz, John Bocco/Peter Ssenyonjo, Mrisho Ngassa na Ramadhan Chombo ‘Lidondo’.

 

Kituko katika mchezo wa leo,

Jamaa mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, alikatiza katikati ya uwanja muda mchache kabla ya mpira kuanza na kwenda kumkumbatia Mshambuliaji wa Azam FC na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars, Mrisho Ngassa, kama alivyofanya kijana aliyekwenda kumkumbatia mshambuliaji wa Brazil, Ricardo Kaka.

 

Katika tukio la leo polisi hawakuweza kuchukua hatua yoyote walimuacha kijana huyo akirejea katika nafasi yake na muda mchache kabla ya mpira kuanza akaondoka uwanjani hapo, ulinzi katika uwanja huo ukiwa hafifu, baada ya mpira kuisha mashabiki mbalimbali waliingia uwanjani kwa lengo la kumgusa mchezezaji huyo pamoja na Ramadhan Chombo, Jabir Aziz na John Bocco.

 

Kutokuwa makini kwa walinzi wa viwanja vya mikioani kutakuja kuleta madhara kwa wachezaji na hata viongozi mbalimbali wa mpira, ikiwa mtu asiye mwema akatokea kuwadhuru.