Kukosa bahati kwa wachezaji wa Azam FC kumepelekea kugawana pointi na timu ya JKT Ruvu baada ya kutoka suruhu katika mchezo wa 6 ligi kuu uliochezwa katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

“Nafasi walizokosa wachezaji wetu zimetupotezea pointi mbili, tulipata nafasi nzuri sana lakini hazikuwa bahati yetu” Kocha mkuu wa Azam FC alitamka maneno hayo baada ya kutoka suluhu na timu ya JKT Ruvu.

Itamar anasema mchezo ulikuwa mgumu sana , timu zote zilicheza kwa kasi na kuviziana mara kwa mara hadi kupelekea kutoka na matokeo hayo yaliyopelekea timu hizo kugawana point moja moja.

“Haikuwa mechi rahisi kama wanavyofikiria, ni mechi ngumu sana tuliyokutana nayo leo, timu imejitahidi kadri ya uwezo wake lakini haikufanikiwa kupata goli, tunashukuru kwa matokeo hayo kuliko tungepoteza mchezo wa leo” anasema Itamar.

Anasema kutokana na mechi hiyo watajipanga zaidi kwani timu itakuwa katika mapumziko ya wiki hivyo watatumia muda huo kurekebisha makosa hayo kabla ya kukutana na Majimaji FC katika mchezo wa 7 utakaopigwa mjini Songea, Oktoba 14.

Azam FC walilazimika kutoka sare hiyo ya bila kufungana kwani kila  timu ilicheza kwa kiwango cha juu na kupelekea mechi hiyo kuwa ngumu kwa timu zote mbili.

Kipindi cha kwanza Azam FC walikuwa wa kwanza kufanya mashambulizi ya nguvu, mchezaji John Bocco aliachia shuti kali lililogonga mwamba wa JKT Ruvu na kukosa nafasi hiyo nzuri.

Azam FC waliongeza mashambulizi zaidi katika lango la maafande wa JKT lakini yaliokolewa vyema na golikipa Shaaban Dihile,

Naye golikipa wa Azam FC Vladmir niyonkuru alifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo ya JKT Ruvu.

KIpindi cha pili kila timu iliingia kwa matumaini ya kuzui kuruhu goli huku wakitafuta goli la ushindi, dakika ya 46 JKT Ruvu walifanya mabadiliko ya kwanza baada ya kumtoa Abdalah Bunu na nafasi yake kuchukuliwa na Sostenes Manyasi.

Dakika ya 60 Mrisho Ngassa alikosa goli la wazi baada ya kuwatoka mabeki wa JKT Ruvu Shaibu Nayopa na Damas Makwaiya lakini akiwa yeye na kipa akaachia shuti jepesi lilidakwa na golikipa Dihile.

Naye mchezaji Mutesa Mafisango alikosa goli zuri baada ya kushindwa kuunganisha mpira mzuri wa Ramadhani Chombo ‘Ridondo’ katika dakika ya 62,  pia dakika ya 88, Chombo alikosa goli baada ya mabeki wa JKT kuuondoa katika eneo la hatari.

Ili kuimarisha timu yao Azam FC walifanya mabadiliko kwa kuingia Jamal Mnyate aliyechukua nafasi ya Seleman Kassim Selembe huku Jabir Aziz akichukua nafasi ya Mutesa Mafisango.

Mwamuzi wa mchezo huo Klina Kabala alichezesha kwa kufata sheria zote za mpira wa miguu kwa kutoa maamuzi sahihi yasiyoumiza timu yoyote.

Katikati mwa kipindi cha pili mwamuzi alitoa kadi ya njano kwa mchezaji wa JKT Ruvu Kisimba Luambano baada ya kumchezea vibaya John Bocco.

Katika mchezo huo mbali na Vladimir, wachezaji Ridondo na Ngassa walicheza katika kiwango cha juu wakifuatiwa na Mafisango Bocco huku Nyoni, Agrey na Shikanda wakitoka kama walinzi bora.

Kwa matokeo hayo Azam FC itakuwa ina pointi saba ikiwa imefungwa michezo mitatu, ikatoka sare mchezo mmoja na kushinda michezo miwili, wakati JKT Ruvu watakuwa na jumla ya point 11 wakishika nafasi ya tatu huku Azam FC watakuwa wamevuka nafasi moja na kuwa katika nafasi ya sita.

Kikosi cha Azam FC kilichoshuka dimbani ni  Vladimir, Shikanda, Mau Ally, Aggrey Morrice,  Nyoni, Mafisango/Jabir Aziz, Seleman Kassim ‘Selembe’/ Jamal Mnyate, Salum Aboubakar ‘Sure boy’, Bocco, Ngassa na Rama Chombo.

 

 

Nyota 6 wa Azam FC waitwa Stars

Kiwango kizuri cha wachezaji wa Azam FC kimepelekea kuchaguliwa kwa wachezaji 6 kuunda timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayojiandaa kucheza mchezo wake wa pili wa kifuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika 2012.

Wachezaji Mrisho Ngassa, Jabir Aziz, Erasto Nyoni, Aggrey Moris, Seleman Kassim ‘Selembe’ na John Bocco ndio walichaguliwa kuunda kikosi hicha wachezaji 23.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan B Poulsen ametangaza kikosi hicho leo kitakachoingia kambini Oktoba Mosi tayari kwa maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa Oktoba 9 katika uwanja mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam .

Wachezaji wengine walioitwa kuunda kikosi hicho ni Shaaban Kado, Juma Kaseja, Said Mohamed, Nadir Haroub, Shadrack Nsajigwa,Haruna Shamte, Salmin Kassim, Stephano Mwasika, Shaaban Nditi, Nurdin Bakar, Nizar Khalfan, Mohamed Banka na Mussa Hassa Mgosi.

Kocha amewaita wachezaji wapya, Mohamed Banka, Haruna Shamte, Salmin Kiss na Salum Machaku katika kikosi hicho kinachoundwa pia na wachezaji wa kimataifa, Danny Mrwanda, Henry Joseph, Nizar Khalfan na Idrissa Rajab.

Amewaacha Jerryson Tegete, Juma Jabu, Abdulhalim Humud, Salum Kanon na Jackson Chove, Stars ilicheza mchezo wake wa kwanza katika mashindano kwa kutoka sare ya 1-1 na timu ya Algeria, mechi za kufuzo kuwania nafasi hiyo zitakamilika Septemba 2011.