Goli la mchezaji Patrick Mutesa Mafisango  la dakika ya 90 lilitosha kuipa Azam FC pointi zote tatu na hivyo kuirejesha kwenye morali ya ushindi ambayo ilikuwa imeanza kupotea.

 

Morali hiyo ilionekana dhahiri shahiri kuanza kupotea baada ya Azam FC kupoteza mechi tatu mfululizo za ligi kuu ya Tanzania .

 

Mafisango ameipatia pointi hizo katika mchezo wa tano wa ligi kuu ya Vodacom VPL na hivyo kuifanya Azam FC kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Mkwakwani kwa kuifunga Africa Lyon 2-1.

 

Katika mchezo huo Azam FC walitawala kipindi cha kwanza na hata cha pili walicheza vizuri sana lakini hawakuwa makini katika kulenga mashuti golini.

 

Azam FC walipata kona ya kwanza katika dakika ya 5 ya mchezo iliyopigwa na Mafisango lakini haikuweza kutoa matunda.

 

Mipango ya kutafuta pointi hizo muhimu ulianza katika dakika ya 29 baada ya mchezaji Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kuandika goli la kwanza kwa Azam FC baada ya mabeki wa African Lyon kufanya uzembe golini kwao.

 

Matokeo hayo yalizidi kuingezea nguvu timu ya Azam FC kwani waliweza kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara, huku mchezaji John Bocco akikosa magoli ya wazi katika dakika ya 16 na 18 wakati Mafisango alikosa dakika ya 19.

 

Jitihada za Azam FC katika kipindi cha kwanza ziliwapeleka mapumziko wakiwa wanaongoza kwa 1-0, huku Lyon wakiwa wamefanya mashambulizi machache ambayo dakika ya 14, Idrissa Rashid na dakika ya 21 Sultan Kitu walikosa magoli ya wazi.

 

Tathmini ya kipindi cha kwanza Azam FC walipata jumla ya kona 7 na mpira wa adhabu ‘faulo’ karibu na goli ulikuwa mmoja wakati African Lyon waliweza kupata kona 3 na kucheza faulo karibu nna goli mara mbili.

 

Kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kasi huku Lyon wakiwa wamebadilika kwa kuanza kutafuta nafasi ya kurudisha goli.

 

Badae timu zote zilifanya mabadiliko kwani katika dakika ya 53 Azam FC walimtoa nahodha msaidizi Ibrahim Shikanda aliyekabidhi nafasi hiyo kwa nahodha mkuu Salum Swedi, pia akaingia Jamal Mnyate na kutoka Seleman Kassim ‘Selembe’.

 

Kwa upande wa Lyon walitoka Benedictor Jacob na kuingia Adam Kingwande, mabadiliko hayo yaliimarisha timu ya Lyon kwani Kingwande aliweza kusawazisha goli hilo katika dakika ya 61 baada ya kuunganisha krosi ya mchezaji Samweli Ngassa.

 

Sare hiyo ilidumu kwa takriban dakika 29 baada ya Mafisango kuinua benchi zima la Azam FC baada ya kuandika goli hilo ambalo limefufua matumaini mapya kwa timu hiyo.

 

 

Azam FC imefikisha pointi 6 kwa shinda mechi mbili na kupotea mechi tatu, ikiwa imecheza mechi tano.

 

Azam FC, Vladimir , Shikanda/Swedi, Mau Ally, Erasto, Aggrey, Mafisango, Selembe/Mnyate, Salum Aboubakar, Bocco, Ngassa, na Chombo.

 

 

 

Sijaridhishwa na kiwango cha wachezaji: Itamar

 

Licha ya kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya African Lyon , Kocha mkuu wa Azam FC amesema ameridhishwa na matokeo hayo kwa kupata pointi tatu muhimu japokuwa timu yake haikufanya vizuri.

 

“Tumepata pointi tatu, lakini sikupendezewa na kiwango walichocheza wachezaji wangu, kunawakati walikuwa wakipoteza muelekeo na kuwapa nafasi timu pinzani, walishindwa kurudisha mipira iliyokuwa ikipotea mara kwa mara alisema Itamar.

 

Anasema timu imefanikiwa kuvuka katika mechi yake ya tano, ikiwa imepoteza mechi tatu muhimu, wanafanya matayarisho zaidi kwa ajili ya mechi ya sita dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa katika uwanja huo huo.

 

Timu imebaki Tanga kwa maabdalizi ya mchezo huo, ambao kocha anaamini utakuwa mchezo mgumu pia kwani JKT ni timu nzuri na imeanza  vizuri katika mechi zake za ligi kuu.