Siku nne baada ya kupoteza mechi zake nne za ligi kuu, Timu ya Azam FC imeondoka leo kuelekea mkoani Tanga (nyumbani kwao) kwa ajili ya maandalizi ya mechi dhidi ya African Lyon inayotarajiwa kuchezwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani.

 

Azam FC ikiwa na kikosi cha wachezaji 23 wameondoka leo mchana tayari kwa maandalizi hayo wakiwa mkoani humo, Mratibu wa timu hiyo Mohamed Seif 'King' amesema timu inaondoka ikiwa na maandalizi ya kutosha.

 

“tunaenda kufanya maandalizi zaidi kwa ajili ya mechi hiyo, tumeamua kwenda mapema ili kuweza kuuzoea uwanja huo na hali ya hewa ya Tanga” amesema King.

 

King ameongeza kuwa kikosi kinachoondoka kitakuwepo mkoani humo kwa kucheza mechi mbili, moja dhidi ya African Lyon na nyingine dhidi ya JKT Ruvu siku ya Jumatano ijayo.

 

Amesema wachezaji wengine wameachwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeruhi, wagonjwa na sababu zinginezo.

 

King amewataja wachezaji watakoenda kuwa ni magolikipa Vladmir Niyonkuru, Jackson Chove na Daudi Mwasongwe, wengine ni Ibrahim Shikanda, Mau Ally, Aggrey Moris, Erasto Nyoni, Mutesa Mafisango.

 

Wengine ni Jabir Aziz, Aboubakar Salum 'Sure Boy', Mrisho Ngassa, Ramadhan Chombo, John Bocco, Haji Nuhu, Tumba Swed, Himid Mao, Salum Swed, Faraj Hussein, Ibrahim Jeba, Peter Senyonjo, Jamal Myate, Seleman Kassim 'Selembe' na Ally Mkuba Sisoko.

 

Wanaobaki ni Ally Manzi, Philip Alando, Malika Ndeule, Ibrahim Mwaipopo na Kally Ongala

 

Mwisho.

 

Mrwanda ajifua na Azam FC

 

Mshambuliaji wa kimataifa wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' na klabu ya Dong Tan ya nchini Vietnam, Danny Mrwanda leo amefanya mazoezi ya kujiweka sawa na kikosi cha Azam FC katika uwanja wa Kines uliopo Manispaa ya Kinondoni.

 

Mrwanda aliyepo nchini kwa mapumziko ya mwezi mmoja, amesema ameamua kufanya mazoezi na Azam FC kwa kuwa amependa program yake ya mazoezi ambayo itamsaidi kwa kipindi atakachokuwa nchini.

 

“Mpira ni kufanya mazoezi yanayoendana na program inayoeleweka, nimeangalia timu zote zilizopo jijini kwa sasa nikaona Azam FC inanifaa kwa mazoezi yangu pindi nitakapokuwepo nchini” amesema Mrwanda.

 

Mrwanda ameongeza kuwa Azam FC inawachezaji wengi walio na uwezo hivyo kufanya nao mazoezi ni sehemu kubwa ya kujipima na kujiongezea uzoefu zaidi.

Amesema kwa kipindi atakachokuwepo nchini ametakiwa kufanya mazoezi na klabu yoyote ya ligi kuu ili kwenda sawa na program za mwalimu wa timu ya Taifa Stars, Jan B Poulsen ili kuona uwezo wake kwani wachezaji wote wapo katika mechi za ligi

 

Naye mratibu wa Azam, Mohamed Seif 'King' amesema timu haikuwa na sababu ya kumkatalia mchezaji huyo kufanya mazoezi, kwani ni mchezaji wa timu ya Taifa.

 

“Tumemruhusu acheze kwani ni mchezaji mzuri, tunatambua mchango wake timu ya taifa, ni moja ya wachezaji wa kimataifa, hivyo tunamkarisha muda wowote aje kufanya mazoezi na sisi.” amesema King.

 

Mrwanda yupo nchini baada ya kumaliza msimu wao wa ligi kuu August 22, huku wakiwa katika nafasi ya nne katika ligi inayojulikana kama V-League.