Timu ya soka ya Azam FC baada ya kufanya usajili wa uhakika washabiki wengi wa soka la bongo walitarajia kwamba ingekuwa ikitoa dozi za uhakika kwa kila timu itakayokatiza mbele yake.

Matarajio hayo yalitokana na ukweli kwamba Azam FC licha ya kukusanya nyota mahiri wa ukanda huu wa Afrika Mashariki, lakini pia ina kocha mzuri, vifaa bora vya kufanyia mazoezi, haina migogoro na haina tatizo la kifedha kuweza kuiandaa timu na kulipa mishahara ya wachezaji na watendaji wa timu.

Hatimaye ligi kuu ya Tanzania Bara maarufu kama VLP ikaanza na Azam FC ikaanza kwa kuipa kichapo cha 2-0 AFC ya Arusha, wengi tukaamini kwamba zile dozi ndiyo zimeanza rasmi

Lakini katika mchezo wake wa pili Azam FC ikapoteza kwa kufungwa 2-1 na Simba SC huku nyota wake John Raphael Bocco ambaye katika mechi ya kwanza alianza kwa kufunga (double) akitolewa nje kwa kadi nyekundu, gundu hilo la kufungwa na Simba SC likasafiri na Azam FC hadi katika miji ya Mwanza na Bukoba ambako Azam FC iliambulia vichapo vya 1-0.

Bahati nzuri nimefanikiwa kuangalia michezo mitatu iliyochezwa Arusha, Tanga na Mwanza kati ya hii minne na baada ya kutafakari kwa kina, ufuatao ndiyo mtazamo na tathmini yangu ya ujumla nikitoa sababu kwa nini Azam FC imepoteza michezo mitatu mfululizo!!

Kupoteza mchezo dhidi ya Simba SC

Mchezo wa mpira wa miguu ni wa ajabu sana, kuna mechi ambazo timu lazima ishinde ili kujenga morali ya ushindi na kama timu ikipoteza mechi hizo basi mambo huwa magumu sana, Ivory Coast, Italy, Cameroon, Uingereza, na Ufaransa zilikumbana na tatizo kama hili kwenye WOZA 2010. Au tunaweza kusema Ghana na Uruguay zilikutana na faida hii niliyoieleza hapo juu. Azam FC ilipaswa kuifunga Simba SC ili kutengeneza hali ya kujiamini lakini baada ya kipigo, kulikuwa na kiwingu cha majonzi yaliyopelekea timu ucheza chini ya kiwango katika mechi iliyokuwa ikifuata siku nne tuu baadaye kwenye uwanja wenye hali ya hewa tofauti na wenye kumbukumbu mbaya kwa Azam FC kwani tangia kuanzishwa kwake haijawahi kushinda Kaitaba. Yakatokea yaliyotokea

Ratiba ngumu ya VPL

Tumeshuhudia makocha kama Arsene Wenger, na Alex Ferguson, Mourinho nk wakiwa wakali na wakilalamikia wapangaji wa ratiba za English Premier League hasa kama watapangiwa mechi chini ya siku nne baada ya kucheza mechi ya ugenini na timu za Big 4. Au baada ya kutoka kwenye michezo ya Uefa Champions League, Kwa nini? Sababu ni kama kilichoikuta Azam FC. Baada ya kufungwa na Simba SC Azam FC ilihitaji muda wa kutosha kuweza kusahau yaliyopita na kurudi katika hali ya mchezo hasa kisaikolojia, unapoingia uwanjani na mawazo ya kichapo ni rahisi sana kufungwa, ni kama mtu aliyeumwa na nyoka, hawezi kwenda vichakani na kutembea pekeyake, atasikia kila sauti za wadudu na ataogopa kila kitu. Lakini kama Azam FC ingeshinda mechi yake na Simba hali ingekuwa ni tofauti kabisa.

Ratiba hii ikaendelea kwenye mechi ya tatu ambapo Azam FC ikalazimika kucheza na Toto Africans siku tatu tuu baada ya siku ilipopokea kichapo toka kwa Kagera Sugar, hapa nilikuwa uwanjani na niliona jinsi wachezaji walivyokuwa nje ya mchezo, wengi wanadhani eti walikuwa hawajitumi lakini mimi nadhani ni sababu hii. Katika mazingira kama haya, Azam FC ilihitaji mtu wa saikolojia kuwaweka sawa wachezaji lakini pia wachezaji walipaswa kujiamini na kuacha kuogopa kulaumiwa au kujilaumu endapo wangepoteza. Azam walikuwa wakicheza kwa umakini sana, hawakujiachia, hawakuwa huru, Ni wachezaji sita tuu kipa Vladmir, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Patrick Mafisango, Mrisho Ngasa na Ramadhani Chombo ambao walionekana kuwa sawasawa kiakili uwanjani na kucheza soka lao.

Hali ya kushindwa kujiamini ilipelekea hata Patrick Mafisango kukosa penalty dakika ya 89 ya mchezo, mwenyewe anasema hakumbuki ni lini mara ya mwisho alikosa penati. Lakini kwangu mimi kama mfuatiliaji wa soka, soka linahitaji kujiamini ndiyo maana hata Ghana walishindwa kufunga penati zao dhidi ya Uruguay sababu baada ya Asamoah kukosa penati yake ya mwishoni mwa mchezo morali ya timu ilishuka ghafla, Uruguay walipata nguvu na Ghana walipata mfadhaiko wa mawazo. Kama ukiwaita leo wachezaji walewale huenda watakupa matokeo tofauti.

Kukosekana kwa John Bocco

Wengi wanaweza wasielewe maana halisi kwani watasema mbona Azam FC kuna Ngasa, Kaly, Senyenjo nk kwenye safu ya ushambuliaji? Who is Bocco? Lakini amin nawaambieni kila timu ina nyota wake na kwa Azam FC Star wa timu ni John Bocco. Binafsi naweza usema ndiye mchezaji anayetoa matumaini kwa kila mtu kambini. Mahusiano yake na viongozi, wachezaji wenzake, nidhamu yake, umakini na kujitolea kwake kwa timu kunamuweka Bocco kwenye daraja moja na Nadir Canavaro pale Yanga, Juma Kaseja pale Simba, Shaabani Nditi pale Mtibwa, Stephen Gerald pale Liverpool, John Terry JT pale Chelsea au Carles Puyor pale Barcelona. Bocco anajua mfumo wa uchezaji wa Azam FC na wachezaji wenzake wanajua namna ya kumchezesha. Katika mechi dhidi ya Toto African, Bocco angeweza kufunga hata Hat-trick

 

Majeruhi

Azam FC ilimpoteza Aggrey Morris kutokana na kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya AFC, huku Ibrahim Mwaipopo na Ibrahim Shikanda wakiwa ni majeruhi. Kwa hiyo kwenye mechi yake dhidi ya Simba SC ukuta wa Azam FC ulicheza bila nguzo nne muhimu kati ya Tano, Ni Erasto Nyoni pekee aliyekuwepo siku hiyo, beki wa kulia na nahodha shikanda akiwa ni majeruhi, beki wa kushoto mwenye uwezo wa kucheza deep midfield Mafisango Patrick alikuwa safarini DRC, Libero Aggrey Morris alikuwa anatumikia adhabu, na Ibrahim Mwaipopo akiwa ni mgonjwa. Hii ilikuwa sababu tosha kwa Simba SC kupata faida na kushinda mchezo wake lakini waliposafiri, Malika ambaye ni mbadala wa shikanda upande wa kulia naye aliumia, huku timu ikimkosa Bocco kutokana na kuwa na kadi. Erasto Nyoni Mashine na Aggrey Morris nao waliumia licha ya kulazimika kucheza wakiwa wajeruhi. Hakuna timu duniani inayoweza kushinda mechi ngumu za ugenini katika mazingira kama haya tena kwa ratiba niliyoieleza hapo juu

 

Nini Kifanyike

Kwanza ni muhimu kuelewa kwamba hadi sasa hakuna timu ambayo haijapoteza pointi, safari ndiyo kwanza inaanza. Imani yangu ni kwamba Benchi la ufundi la Azam litatuliza kichwa na kurekebisha kasoro zilizopo. lakini lazima tutambue kuwa ligi ni ngumu sana na kila timu msimu huu ni Nzuri, Yanga ilishinda kimazabe dhidi ya Polisi Tanzania na Jana nilishuhudia uwezo wa timu ile ilipocheza na kuichapa Simba SC, nilishuhudia mechi kati ya Yanga na Mtibwa na hakika sinabudi kusema soka letu limepiga hatua kubwa sana. walioiona Simba vs Ruvu Shooting wanasema licha ya kufungwa Ruvu ndiyo iliyocheza. Tayari nimeiona JKT Ruvu na amin nawaambia mwaka huu hapatoshi

Azam FC bado ina nafasi kubwa ya kitimiza malengo yake. Azam FC inapaswa kutumia mfumo uleule wa 4-3-3 na kuacha kufanya majaribio ya mifumo kwenye ligi kama huu wa 4-4-2. hakuna muda wa kupangua kikosi eti kwa sababu tumefungwa 2-1, 0-1 na 0-1. Naamini endapo John Bocco na Ibrahim shikanda watarudi hali itabadilika na wataendelea kutupa raha

Goo…. Azam FC Go….