Maamuzi mabovu ya mwamuzi Mathew Akrama yamepelekea timu ya Azam FC kupoteza mchezo wake wa pili dhidi ya Simba SC kwa kuruhusu kufungwa 2-1 katika mchezo uliochezwa uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

 

Katika mchezo huo mwamuzi huyo aliweza kutoa maamuzi ya upendeleo wa wazi kwa kikosi cha Simba kwani dakika ya 12 ya mchezo mchezaji wa Azam FC, John Bocco alipewa kadi nyekundu katika mazingira ya kutatanisha.

 

Mwamuzi huyo alitoa kai hiyo baada ya kutokea mchezaji Joseph Owino akiwa chini baada ya kusukumana na Bocco wakiwania mpira wa juu.

 

Kutolewa kwa Bocco kulipelekea timu ya Azam FC kuongeza nguvu na kucheza kwa kasi zaidi kwani dakika nne baadaye Mchezaji Ramadhan Chombo ‘Ridondo’ aliweza kuandika goli kwa kupiga kichwa kilichomuacha kipa Ally Mustapha na kutinga wavuni.

 

Baada ya goli hilo mwamuzi huyo alizidi kuitetea Simba kwa kipindi chote kilichobaki na kupelekea timu hiyo kuweza kusawazisha  goli hilo kwa mpira uliozidi ‘offside’.

Goli hilo lililofungwa dakika ya 46 na nahodha wa timu hiyo Nico Nyagawa, baada ya mwamuzi kuamuri faulo tatanishi na Nico Nyagawa akiwa offside aliusukuma mpira golini na kusababisha zogo kwa dakika kadhaa

Azam FC  katika kipindi cha kwanza ilionyesha kandanda safi na mchezo wa kiwango cha juu kwani iliweza  kutawala mchezo kwa huo kwa takriban kipindi chote cha kwanza.

 

Kipindi cha pili Azam FC walianza kwa kasi na kuipeleka puta Simba ambao walionekana kupoteana na kutegemea msaada ya refarii pekee, Azam FC ilifanya mabadiliko ya kwanza dakika ya dakika ya 60 kwa kumtoa Ramadhan Chombo ambaye alipewa kadi ya njano na nafasi yake kuchukiwa vyema na kiungo mshambuliaji mahiri Seleman Kassim ‘Selembe’.

Dakika ya 56 Simba walipata goli la ushindi kupitia kwa mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’. Goli hili lilikuwa la kuotea dhahiri kwani mshika kibendera alikuwa ameshanyanyua juu kibendera chake kuashiria kuwa Mgosi alikuwa ameotea lakini baada ya goli kuingia alishusha kibendera na kusababisha ubishani uliosababisha kipa wa Azam Vladmir naye kuoneshwa kadi ya njano,

Baada ya goli hilo timu zote zilifanya mabadiliko mengine kwani Azam FC walimtoa Kally Ongala na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Ssenyonjo huku Tumba Swed akachukua nafasi ya Malika Ndeule.

 

Azam FC Vladimir, Malika/Tumba, Mau Ally, Salum Swed, Erasto Nyoni, Salum Aboubakari ‘Sure Boy’, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, Kally Ongala/Peter Senyonjo na Ramadhan Chombo/Seleman Kassim.

 

Simba, Ally Mustapha, Salum Kanon, Amir Mftah, Joseph Owino Kelvin Yondan, Jerry Santo, Nico Nyagawa, Mohamed Banka, Emmanuel Okwi, Mussa Mgosi, na Uhuru Seleman.

 

 

Itamar: Mpira wa Tanzania hauta kua.

Baada ya maamuzi ya mabovu ya mwamuzi wa mchezo kati ya Azam FC na Simba, kocha mkuu wa Azam FC Itamar Amorim amesema kwa maamuzi ya aina hiyo katika mechi za ligi kuu kutapelekea soka la nchi kubaki kama lilivyo.

 

Itamar amesema hayo baada ya mwamuzi huyo kutoa maamuzi ya pendeleo ya ya wazi kwa timu ya Simba.

“kwa maamuzi haya timu za Tanzania zitaendelea kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa kwani wamezoea kupendelewa  katika mechi na wanapokutana na waamuzi wakimataifa huishia kuwa washiriki tu. Angalia jinsi walivyochezesha, unadhani Simba ikienda kwenye michezo ya kimataifa itapata mwamuzi kama huyu? na kama haitapata unadhani nini kitatokea? alihoji Itamar.

Itamar amesema  waamuzi wa Tanzania wanahitajika kubadilika ili kusaidia kukuza mpira wa Tanzania. Hata wao wenyewe wanahijtaji kutenda haki na kujiendeleza ili tupate waamuzi kwenye kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika toka Tanzania, angalia wanavyochezesha ndiyo maana hatupeleki waamuzi kwenye mashindano makubwa alisema Itamar.

 

Akizungumzia mchezo huo kocha Itamar amesema timu yake imecheza vizuri kuliko Simba, wameweza kutumia mapungufu ya Simba kwa nyakati tofauti lakini maamuzi ya mwamuzi huyo ndio yaliyowaangusha.

 

Kondo: Waamuzi wanaharibu mchezo

Kocha msaidizi wa Azam FC Habib Kondo amesema maamuzi yasiyosahihi ya waamuzi mbalimbali hapa nchini yanaharibu mazingira ya mchezo.

Kondo amesema waamuzi wanashindwa kufuata kanuni 17 za mpira wa miguu  hali inayopelekea kutotendewa haki kwa baadhi ya timu huku wakizisaidia baadhi ya timu.

“waamuzi wanabeba timu za Simba na Yanga, bila kuangalia muelekeo wa ligi, maamuzi yao yanaumiza timu zingine, na kama watachezesha kwa kufuata misingi yote kila timu ingepata nafasi”. Amesema Kondo.

 

Salum Swed: Hatujakata tamaa

 

Nahodha wa timu ya Azam FC, Salum Swed amesema kupoteza kwa timu hiyo katika mechi yake dhidi ya Simba hakutapoteza malengo yao ya kuwa katika nafasi za juu.

 

Swed amesema matokeo ya mechi hiyo hayakuwa sahihi kwani mwamuzi alikuwa anaegemea upande mmoja wa maamuzi yake.

 

“Tumecheza vizuri japo tulikuwa pungufu, tumejitahidi kwa ajili ya kushinda mechi hii lakini tumepoteza kwa sababu za mwamuzi wa mchezo huo, lakini hatujakata tama kwani ligi ndio imeanza, tunauhakika tutafanya vizuri mechi zijazo”  Swed.