Kikosi kamili cha wachezaji 23 wa Azam FC kitaondoka alfajiri ya kesho Alhamisi kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya pili ya ligi kuu dhidi ya Simba SC itakayochezwa siku ya jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

 

Wachezaji walioachwa katika msafara huo Ibrahim Mwaipopo Popo's anayekabiliwa na maumivu ya nyama za paja, Philip Alando, Ally Manzi na Haji Nuhu.

 

Mratibu wa timu Mohamed Seif 'King' amesema kikosi kilichoteuliwa kitakuwa cha safari tatu ambazo kitacheza mechi tatu ambazo ni dhidi ya Simba, Kagera Sugar utakaochezwa siku ya Jumatano, Sept 15, mjini Kagera na dhidi yaToto Africans utakaochezwa Sept 18 jijini Mwanza.

 

King amewataja wachezaji watakaokuwa katika msafara huo kuwa ni Vladmir Niyonkuru, Salum Swed, Tumba Swed, Ibrahim Shikanda, Ibrahim Rajab 'Jeba', Jabir Aziz, Mrisho Ngasa na Kali Ongala.

 

Ramadhan Chombo, Daud Mwasongwe, Erasto Nyoni, Mau Ally, Salum Aboubakar, Malika Ndeule, Seleman Kassim 'Selembe', Peter Ssenyonjo, Patrick Mutesa Mafisango na Agrey Morris.

 

Viongozi ni King Mwenyewe, Meneja Ibrahim Hamad, Daktari msaidizi Twalib Mubaraka, kit manager Khamis na mchua misuli Mbembe, Kocha mkuu Itamar Amorim na makocha wasaidizi Kondo na Iddi Aboubakar.

 

King amesema kikosi hicho kitarejea Dar es Salaam mara tu baada ya mechi hiyo kumalizika tayari kwa maandalizi ya safari ya kuelekea Kagera siku ya Jumapili asubuhi.

 

Redondo: Ushindi Lazima

 

Zikiwa zimesalia siku chache kuelekea katika mpambano mkali kati ya Azam FC na Simba SC, mchezaji Ramadhani Chombo 'Redondo' wa Azam FC amesema ushindi lazima kwa Azam FC.

 

“Hii ni moja ya mechi nzito kwangu, na ni mechi ya kawaida kwani nipo Azam FC kucheza na na kuihakikishia ushindi timu yangu ya Azam, hivyo mashabiki wa Azam FC wasiwe na hofu kwani kwa sasa nawatumikia wao” amesema Redondo.

 

Redondo anasema yeye na wachezaji wengine wageni wamekuja Azam FC kufanya kazi, na kuhakikisha timu inafanya vizuri kwa kushinda mechi zake bila kuangalia wametoka timu gani.

 

Redondo anajivunia kikosi chao kwa kusema “Tuna kikosi kizuri na kamili kwa ajili ya mechi zetu za ligi kuu.” anasema Redondo.

 

Mechi itachezwa siku ya jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani ulioko mkoani Tanga.

 

Swedi: Tunangoja point tatu kwa Simba

 

Nahodha wa Azam FC Salum Swedi amesema atahakikisha timu yake inatoka na ushindi wa pointi tatu katika mechi na Simba itakayochezwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

 

Swedi amesema Azam FC ya mwaka huu ni tofauti na ile ya mwaka jana, kwa kuwa ina wachezaji mahiri na wazuri ambao wameonyesha uwezo mkubwa wa kuleta upinzani katika ligi kuu.

 

“timu zote zimefanya usajili, ila Azam FC imefanya usajili mzuri wenye uhakika wa ushindi kwa kila mechi, tumecheza na Simba mwaka jana wakatufunga, mwaka huu tukatoka nao sare katika mechi ya kirafiki, kwa matokeo hayo jumamosi hawatoki” anasema Swedi

 

Nahodha huyu mstaafu wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' anasema japo katika mechi kuna matokeo matatu, kufunga, kufungwa na kutoka sare, Azam FC imejiandaa kutoka na ushindi huo kwa sababu itakuwa ikicheza nyumbani.

 

Swedi amewataka wakazi wa Tanga kuwapa mshikamano kwa kuwa wamechagua uwanja huo kama uwanja wa nyumbani.

 

Nyoni: Matumaini ni ushindi tu

 

Beki wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' na Azam FC, Erasto Nyoni ameongeza matumaini ya ushindi kwa timu yake katika mechi yao ya pili dhidi ya Simba SC, itakayofanyika siku ya Jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

 

Nyoni amesema mwalimu Itamar Amorim amewaandaa wachezaji wote kwa ajili ya mechi hiyo na mechi zingine za ligi kuu.

 

“kwa mazoezi tuliyopata, ushindi lazima, kwani Simba tunawajua vizuri na tutatumia nafasi hiyo kujiwekea mazingira mazuri katika ligi kuu, kwa kutoka na ushindi.” amesema Nyoni.