Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeshauriwa kuweka uzalendo mbele wakati watakapokuwa mchezoni dhidi ya Aljeria, hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera.

 

Bendera Alisema Watanzania wanataka ushindi dhidi ya Algeria ambayo ni timu ngumu kwenye mchezo wa Ijumaa  ambao utakuwa wa kwanza wa Kundi D la kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Afrika mwaka 2012.

 

Bendera aliwashauri wachezaji hao wanaoondoka leo na shirika la ndege la Quatar Airways kuhakikisha wanajituma na kutambua wamekomaa katika mashindano makubwa kama hayo, akieleza kuwa ni vyema wakaonyesha mabadiliko ili kuiletea sifa  nchi yao katika medani ya soka.

 

Kwenu ninyi hii ni fursa muhimu kwani kuna wachezaji mwengine wengi wazuri kama ninyi lakini wamekosa nafasi kwenye kikosi hiki alisema Joel

 

Tenga amshukuru Bendera

 

Wakati huohuo Rais wa Shirikisho la Soka  Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amempongeza waziri Bendera kwa kuwa bega kwa bega na TFF tangu alipoteuliwa kuwa naibu waziri mpaka sasa anapomaliza muda wake na kumtaka kuendelea kuwa nao bega kwa bega katika kuileta Tanzania sifa nzuri katika michezo.

 

Pia Tenga aliwaasa wachezaji wa Stars kwenda kuiwakilisha vyema Tanzania na kurudi na ushindi ili waweze kusonga mbele katika michuano hiyo ya kimataifa.

 

NMB, Serengeti wamwaga vifaa vya 56Milioni

wadhamini wakuu wa timu  ya Taifa Taifa Stars, benki ya NMB na Serengeti Breweries (SBL) wametoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Shilingi  56 milioni kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Algeria.

 

Nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema kuwa Watanzania na wadau wengine wa soka nchini wategemee ushindi kwani maandalizi waliyofanya ni mazuri na kule wanakwenda kushindana ili kuweza kuipeperusha vyema bendera ya nchi yao.

 

KOCHA wa Algeria, Rabah Saadane amesema  timu yake haina budi kunyakua pointi zote tatu wakati itakapovaana na Tanzania Ijumaa mjini Blida, lakini akaonya kuwa ushindi utapatikana kwa mbinde kwa sababu wapinzani wao wanaonekana hawaruhusu mabao mengi.

 

Kwa mujibu wa mwandishi Angetila Osiah wa gazeti la hilo la Mwananchi toleo la leo, Algeria, moja ya nchi sita zilizoiwakilisha Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini katikati ya mwaka huu, inapewa nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo ya Kwanza ya Kundi D ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2012.

 

Lakini, kocha huyo hajabweteka na nafasi ya nchi yake kwenye mechi hiyo na katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi usiku, aliweka bayana sababu ambazo zinaifanya mechi hiyo kuwa ngumu.

 

"Kwa kuangalia nafasi yetu kwenye orodha ya ubora duniani, tutakuwa tunapewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini mechi itakuwa ngumu," alisema kocha huyo akikaririwa na gazeti la El Watan. "Pia, ukweli kwamba wapinzani wetu ni wagumu, wameruhusu kufungwa mabao machache.

 

"Wachezaji wangu hawatakuwa kwenye hali nzuri kimchezo. Katika kipindi hiki cha msimu, wachezaji wengi ndio kwanza wameanza mazoezi na klabu zao. Baada ya (fainali za) Kombe la Dunia, wachezaji wengi walienda mapumziko ya wiki tatu hadi nne.

 

"Kwa hiyo hawana wiki zaidi ya mbili tangu waanze mazoezi. Wanahitaji muda zaidi ili kurudi kwenye hali yao ya kimchezo. Ndio maana siishi kusisitiza kuwa kipindi hiki katika mwaka kimchezo kwa kweli ni kigumu sana."

 

 

Pia, katika mkutano huo na waandishi uliofanyika kwenye Uwanja wa Julai 5, kocha huyo alikaririwa na Shirika la Habari la Algeria akisema: "Lengo letu ni kupata pointi zote tatu dhidi ya Tanzania, timu inayoheshimika ambayo hatutakiwi kuidharau.

 

"Tuna matatizo ya kisaikolojia kwa kuzingatia ushiriki wetu kwenye fainali za Kombe la Dunia na nafasi tunayopewa ya kushinda."

 

Kocha huyo alisema anatarajia Algeria kucheza soka la kushambulia dhidi ya Tanzania, ambayo vyombo vya habari vya Algeria vimesema itacheza kwa kujihami wakati wote.

 

Vyombo vya habari nchini Algeria vimekuwa vikiponda uamuzi wa kocha huyo kuhamishia mechi hiyo kwenye Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida hasa baada ya timu ya taifa kukubali kipigo mbele ya Gabon mjini Algiers, lakini Saadane alikuwa na sababu nyingi za kutetea uamuzi wake.

 

"Tutakuwa na mashabiki wa aina yake (kwenye uwanja wa Tchaker). Kila siku ushangiliaji wao husaidia wachezaji kuanzia kwenye michuano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika hadi Kombe la Dunia. Kwa wakati huu hatuna kingine zaidi ya kuhitaji msaada wa mashabiki.

 

Hata hivyo, kocha huyo aliwataka mashabiki kuheshimu timu pinzani na hasa wakati wimbo wa taifa wa Tanzania utakapokuwa ukiimbwa.

 

Kocha huyo pia alijitetea kuwa uamuzi wa kuhamishia mechi mjini Blida pia ulifanywa kwa kushirikisha wachezaji ambao waliuafiki.