Zikiwa zimesalia siku 11 kabla ya mchezo wa pili wa ligi kuu kati ya Azam FC na Simba SC zote za Dar es Salaam, utakaochezwa katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga, timu zote zipo katika maandalizi ya hali ya juu.

 

Mchezo huo utachezwa katika uwanja huo kutokana na matayarisho katika uwanja wa Uhuru, TFF imezitaka timu zote zilizotumia uwanja wa Uhuru kama uwanja wa nyumbani kutafuta viwanja vingine vilivyopo nchini.

 

Baada ya tamko hilo Azam FC wameamua kuchukua uwanja wa Mkwakwani uliopo Tanga kama uwanja wa nyumbani hadi mwezi Novemba.

 

Wakati Azam wakitumia uwanja wa Mkwakwani, Simba watakuwa CCM Kirumba wakati mahasimu wao Yanga wakiwa bado hawajapata uwanja wa kuchezea.

 

Pamoja na hilo, bado Azam FC inawasiliana na TFF kuona uwezekano wa mechi hiyo kuchezwa jijina Dar es Salaam kwenye Dimba la Taifa.

 

Afisa habari wa timu ya Simba, Clifford Ndimbo amesema mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Mkwakwani kutokana na makato makubwa ya matumizi katika uwanja wa Taifa.

 

“Tulipanga kucheza katika uwanja wa Taifa lakini makato ya asilimia 20 ni makubwa, hivyo tutatumia uwanja wa CCM Kirumba uliopo Mwanza kama uwanja wa nyumbani na mechi katika yetu na Azam FC itachezwa mkoani Tanga.” amesema Ndamo.

 

Akizungumzia matayarisho ya mechi hiyo Ndimbo amesema timu yake iko katika hari nzuri ya kuendeleza kutetea ubingwa wake hivyo wanatarajia kupata ushindi katika mchezo huo.

 

Ikiwa ni mara ya pili kwa Azam FC kucheza katika uwanja huo, Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa amesema timu imejiandaa vya kutosha walichokuwa wakisubiri ni taarifa kutoka TFF itakayowajulisha uwanja watakaocheza mechi hiyo.

 

“sisi tupo tayari mechi hiyo ichezwe katika uwanja wa Mkwakwani, tunachosubiri ni kujua mapema ili tufanye maandalizi ya safari kama tutacheza katika uwanja wa Mkwakwani”. Amesema Nassor.

 

Nassor anaongeza kuwa kujua mapema kutatoa muda mrefu wa maandalizi kwa timu kwani baada ya mechi hiyo timu itakuwa katika safari ya kuelekea mkoani Kagera siku inayofata kwa ajili ya mechi yake ya tatu dhidi ya Kagera Sugar.

 

Katibu anasema baada ya mechi hiyo itabidi irudi siku hiyo hiyo tayari kwa kuondoka na ndege ya asubuhi kuelekea mkoani Mwanza ambako watachukua meli na kwenda Kagera.

 

….

 

U20 wafanya vizuri mazoezini

-Muda wa Azam FC, Taifa Stars

 

Siku chache baada ya wachezaji wa Azam FC waliounda kikosi cha timu ya Taifa ya vijana Ngorongoro Heroes, kurejea kuongeza nguvu katika timu yao, wameendelea kufanya vizuri katika mazoezi ya kujiandaa kwa mechi zijazo za ligi kuu.

 

Wachezaji walikuwa katika timu ya U20 ni nahodha Himidi Mao, Salum Aboubakar 'Sure Boy', Tumba Swed, Omar Mtaki (Ngorongoro Heroes) na Ibrahim Jeba aliyekuwa katika timu ya taifa ya Zanzibar 'Karume Boys'

 

Azam FC inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Simba SC, Kocha mkuu wa timu hiyo Itamar Amorim amesema wachezaji wamerudi wakiwa na hari mpya hivyo watafanya vizuri katika mechi zijazo za ligi kuu.

 

Akizungumzia kuwa timu pekee iliyo na wachezaji wengi wanaounda timu ya Taifa ya Tanzania kocha huyo amesema hiyo ni nafasi nzuri kwa timu yake kwani imepata nafasi ambayo haijawahi kuchukuliwa na timu zingine mbali na Simba na Yanga.

 

'Ni mafanikio kwetu kutoa wachezaji wengi watakaokwenda Algeria, huu ni muda wetu kuonesha uwezo wetu na kuchangia timu ya Taifa.” Itamar.

 

Wachezaji wa Azam FC waliopo Taifa Stars ni Jackson Chove, Erasto Nyoni, Aggrey Morice, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, John Bocco na Seleman Kassim 'Selembe'.

 

Stars inaelekea nchini Algeria kuanza mechi ya kwanza ya kufuzu kucheza fainali za kombe la mataifa ya Africa 2012 yatakayofanyika nchini Benin na Equatorial Guinea