Goli la kusawazisha la mchezaji Mrisho Ngassa wa Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' limeipeleka timu hiyo katika sare ya 1-1 na timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam leo.

Ikiwa ni mechi ya kwanza kwa kocha mpya wa Taifa Stars Jan B Poulsen, Taifa Stars ilianza vibaya katika kipindi cha kwanza na kuruhusu goli dakika ya 13 baada ya mchezaji wa Harambee Stars MacDonald Mariga anayecheza AC Millan ya Italia kwa kupiga mpira wa adhabu ulioenda moja kwa moja katika goli la Taifa Stars.

Taifa Stars ilijaribu kurudisha goli hilo kwa kipindi cha kwanza baada ya kumtoa mshambuliaji mahiri Jerryson Tegete na kuingia Mussa Hassan 'Mgosi' katika dakika ya 27 lakini ikashindikana kwani Harambee Stars waliweza kuzuia mashambulizi hayo, na kupeleka timu zote mapumziko huku Harambee ikiongoza kwa goli 1-0.

Kipindi cha pili Taifa Stars ilifanya mabadiliko kwa kuingia Seleman Kassim 'Selembe' na Aggrey Moris waliochukua nafasi za Uhuru Seleman na Kelvin Yondan waliweza kubadilisha mchezo na kutoa mashambulizi mara kwa mara yaliyopelekea dakika ya 57 kupata goli la kusawazisha kupitia kwa Mrisho Ngassa aliyepokea pasi nzuri ya Nadir Haroub.

Matokeo haya yalipelekea timu ya Harambee Stars kufanya mabadiliko kwa kuingia Allan Wanga na Antony Kimani waliochukua nafasi za John Baraza na George Odhiambo, mabadiliko hayo hayakubadilisha matokeo na kufanya timu hizo kutoka sara ya 1-1.

Timu hizo zikiwa zinajiandaa kucheza mechi za kufuzu kucheza fainali za kombe la Mataifa ya Africa AFCON 2012, Taifa Stars itacheza na Algeria wakati Harambee itakutana na Guinea Bisau mapema mwezi ujao katika mchezo wa kwanza wa kuwania kucheza fainali hizo.

Kocha mkuu wa Taifa Stars Poulsen amesema mechi ya leo ameitumia kama sehemu ya kujaribu wachezaji ambao watakuwa katika kikosi hicho ikiwa huu ni mchezo wake wa kwanza kwa kocha huyo baada kuchukua nafsi ya kocha Marcio Maximo aliyemaliza muda wake.

Akitoa tathmini ya mchezo huo Kocha Poulsen amesema “ kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri kwa Taifa Stars kwani walishindwa kutumia nafasi zao vizuri lakini kipindi cha pili walifanya vizuri”.

Amesema kutokana na matokeo hayo anatumaini mechi yake ya pili na zinazokuja timu itafanya vizuri.

Taifa Stars Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Kelvin Yondan/Aggrey Moris, Abdi Kassim/ Athman Idd 'Chuji', Mrisho Ngassa, Nurdin Bakari, Jabir Aziz/Abdulhalim Hamoud, Jerryson Tegete/Mussa Hassan 'Mgosi', Uhuru Seleman/Seleman Kassim 'Selembe', Idrissa Rajab/Stephano Mwasika na Nadir Haroub.

Harambee Stars, Wilson Obugu, George Owino, Julius Owino, Lloyd Wahome, Patrick Mzee/ James Situma, Edgar Ochieng, MacDonald Mariga, George Odhiambo/, Dennis Oliech, John Baraza/Allan Wanga, Kelvin Omondi/Paul Were.