Ikiwa ni siku nne zimepita tangu Azam FC irejee kutoka visiwani Zanzibar ilipoweka kambi ya wiki, siku ya Jumapili inatarajia kucheza mchezo wake wa mwisho wa majaribio dhidi ya timu ya Mtibwa Sugar utakaochezwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Azam FC ilipokuwa visiwani Zanzibar imecheza mechi tatu za kirafiki ikifunga mechi moja dhidi ya mabingwa wa Zanzibar, Zanzibar Ocean view 2-1, ikatoka sare mechi mbili za JKT Ruvu na Simba SC.

Kabla ya kuelekea visiwani humo Azam FC ambayo haijapoteza mechi yoyote ya kirafiki ilitoka sare ya bila kufungana na timu ya Taifa ya vijana Ngorongoro Heroes na kuifunga Ruvu Shooting 2-1.

Azam FC kwenda Arusha Jumanne

Timu ya Azam FC siku ya Jumanne inataraji kuelekea mkoani Arusha tayari kwa kucheza mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya timu ya AFC ya Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kocha wa timu hiyo Itamar Amorim amesema wachezaji wote watakuwa pamoja kabla ya siku ya jumamosi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mwisho kwa safari hiyo ambako wanatarajiwa kucheza August 21.

Itamar amesema hadi sasa timu iko vizuri, amerekebisha makosa yaliyotokea katika mechi zake za majaribio hivyo timu iko tayari kwa ligi kuu.

“katika mechi za majaribio yalionekana makosa machache, nimeshayafanyia kazi hivyo tupo tayari kuanza ligi kuu tukiwa hatuna tatizo lolote” amesema Itamar.

Akizungumzia safari ya Zanzibar Itamar amesema ilikuwa safari ya mafanikio kwa timu kwani imeweza kufanya mazoezi na kucheza katika kiwango cha juu, ikiwa ni pamoja na kuzoeana kwa wachezaji wapya na wageni.

“Wachezaji wameonesha ushirikiano mzuri muda wote walipokuwa Zanzibar wameweza kucheza kama walikuwa pamoja kwa muda mrefu, ushirikiano huo utaisaidia timu kufanya vizuri katika mechi zake za ligi kuu.” amesema Itamar.

Daud Mwasongwa

Katika maandalizi ya ligi kuu leo timu ya Azam FC imefanya mazoezi maalumu kwa magolikipa na wachezaji wote, huku golikipa anayechipukia Daud Mwansongwa akiongoza kufungwa na wachezaji wenzake.

Zoezi hilo lilidumu kwa takribani nusu saa lilimuacha kipa huyo kutoka kikosi cha Azam Academy akifungwa magoli mengi kuliko kipa namba moja wa timu hiyo Vladmir Niyonkuru aliyekuwa akiokoa mipira mara kwa mara.

Beki wa kutumainiwa Salum Swed aliweza kuwafunga Daudi na Vladmir kwa mikwaju aina ya kanzu na kuacha wachezaji wengine wakizidisha nguvu zaidi kuwafunga wenzao.

Wachezaji Kali Ongala, Mohamed Binslum, Patrick Mafisango Ramadhan Chombo 'Lidondo', Philip Alando na Ally Manzi waliweza kuwafunga magolikipa wote wakitumia aina yao tofauti ya ufungaji ikiwemo kuwachenga magolikipa ndani ya eneo la hatari.

Mchezaji Faraji Hussein kwa wakati wake aliweza kumchezea kipa Vladmir na kufanikiwa kumfunga kipa huyo asiyefungika kirahisi.

Katika mazoezi wachezaji 17 walihudhuria mazoezi hayo huku wengine 12 wakiwa katika timu za Taifa za Taifa Stars, Ngorongoro Heroes na Harambee Stars ya Kenya (Ibrahim Shikanda).

Malaria ya msumbua Senyonjo

Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa mazoezini katika uwanja wa Uhuru huku mchezaji Peter Senyonjo akiwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria.

Senyonjo ameanza kuumwa pindi aliporejea kutoka visiwani Zanzibar ambako timu iliweka kambi ya wiki mbili.

Daktari msaidizi wa timu hiyo Habib amesema hali ya Senyonjo inaendelea vizuri kwani amepata matibabu na atarejea uwanjani muda si mrefu.

'Hali yake inaendelea vizuri, anaendelea na matibabu sahihi ya malaria' amesema Dk Habib.