Siku tatu baada ya kuifunga Simba SC 3-2, timu ya Azam FC imeendeeza ushindi kwa kuifunga AFC 5-1 katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa ljana jioni uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam .

 

Azam FC wakiwa na kikosi kamili kilichoiangamiza Simba walicheza soka la kuvutia na wachezaji John Bocco, na Mrisho Ngassa kufunga mara mbili kila mmoja hivyo kuifikisha timu hiyo kuwa na jumla ya pointi 26 katika msimamo wa ligi kuu ya Vodacom.

 

Goli la kwanza kwa Azam FC lilipachikwa wavuni katika dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ aliyeunganisha vema krosi safi ya Mrisho Ngasa toka winga ya kushoto na Bocco kuachia shuti fupi lililompita kipa wa AFC na kuingia moja kwa moja wavuni.

 

Dakika 26 baadaye Ibrahim mwaipopo ilipiga kiufundi krosi iliyowababatiza Ramadhani Chombo na beki wa AFC na kutinga uwanjani, kila mwandishi wa habari alikuwa na jibu lake kuhusu mfungaji wa goli lile ingawa wengi tulikubaliana kuwa goli lilifungwa na aliyepiga shuti kwani wengine mpira uliwagonga kwa bahati mbaya na aliyepiga shuti mpira ule ni Ibrahim Mwaipopo

 

Baadaye Bocco kuongeza goli la tatu katika dakika ya 41 akitumia vizuri uzembe wa mabeki na kipa wa AFC, Ally Mohamed.

 

Matokeo hayo yaliipeleka mapumziko AFC iliyokuwa ikitumia mfumo wa 5-5-2 ikiwa nyuma ya magoli matatu na kuiacha Azam FC iliyokuwa ndani ya 4-3-3 ikiongoza kipindi kizima kabla ya kurejea kipindi cha pili ambacho AFC walianza kwa kucheza vizuri ndani ya dakika moja.

 

 Mchezaji mwenye gharama kuliko wote Tanzania -MVP, Mrisho Ngasa aliongeza maumivu kwa AFC akiifungia Azam goli la nne dakika ya 47 baada ya kuunganisha mpira wa mbali uliopigwa na nahodha Ibrahim Shikanda.

 

Ngassa mchezaji mwenye kasi na uwezo wa kucheza na mpira atakavyo alifunga kalamu ya magoli kwa kupachika goli la tano dakika ya 76 akitumia vizuri mpira aliotupiwa na mshambuliaji Peter Ssenyonjo aliyeingia kuchukua nafasi ya Bocco.

 

Azam FC baada ya kufunga goli hilo la tano, benchi la AFC likafanya mabadiliko ya golikipa alitoka Ally Mohamed na nafasi yake kuchukuliwa na kipa chipukizi Daudi Makungu lakini golikipa huyo hakufungwa hata goli moja.

 

Goli la AFC lilipatikana dakika ya 90 kupitia kwa mchezaji Jimmy Shoji aliyeingia kuchukua nafasi ya Mahsen Bawaziri aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa Emmanuel Panju, kwa matokeo hayo AFC itakuwa timu iliyofungwa magoli mengi katika mzunguko wa pili, hadi sasa kwani katika michezo miwili imefungwa 11-2.

 

Baaada kufunga magoli mawili katika mchezo wa leo, Mrisho Ngassa amefikisha idadi ya magoli 9 na kuongoza wafungaji katika ligi kuu, huku Bocco akiwa na magoli 6 na kuingia rasmi kwenye mbio za kuwania mfungaji bora.

 

Akizungumza dakika chache baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha wa Azam FC, Stewart Hall alisema amefurahishwa kupata pointi tatu lakini timu yake haikucheza kama ilivyocheza mchezo wake uliopita dhidi ya Simba.

 

“Wamecheza katika kiwango cha juu lakini hakijafikia mechi ya Jumapili, mabadiliko yametokea kwa kuwa najaribu kuwachezesha wachezaji wote niwaone viwango vyao ndipo nitakapopata timu maalum.”alisema Stewart.

 

Azam FC Vladimir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Mutesa Mafisango, Erasto Nyoni, Aggrey Moris, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz/Selembe, Salum aboubakar/Jamal Mnyate, Chombo, Bocco/Senyonjo. na Ngassa