Yanga SC v Azam FC; Ni mchuano mkali

Category: 
Team: 
Azam FC

NI mchuano mkali! Ndivyo unavyoweza kusema hivyo, pale Azam FC itakapokuwa ikivaana na Yanga, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam keshokutwa Jumapili saa 10.00 jioni.

Mchezo huo unasubiriwa na mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na upinzani mkali unaoonyeshwa na timu zote mbili kila zinapokutana.

Timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, Azam FC ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mchuano wa kwanza kwa timu zote mbili, ni ule wa kuwania nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, hadi sasa Azam FC ikiwa inaishikilia kwa pointi zake 57 huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu ikijizolea 55.

Aidha jambo jingine linaloongeza mchuano huo, ni kwenye takwimu za timu hizo zilipokutana katika ligi, zinazoonyesha kulingana kila kitu.

Azam FC imekutana na Yanga mara 23 kwenye mechi za ligi, ikiwa imeshinda mara nane kama ilivyo kwa Yanga, zikatoka sare mara saba, huku wababe hao wa Chamazi wakifunga jumla ya mabao 31 na Yanga wakitupia 30.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ameendelea na programu ya kukinoa kikosi hicho kujiandaa na mchezo huo, tokea Jumanne iliyopita, vijana wakionekana kuwa kwenye hali nzuri kabisa.

Mwanzoni mwa wiki hii, kikosi hicho kilizidi kuimarika baada ya kurejea nchini kwa wachezaji wake wawili, beki wa kushoto, Bruce Kangwa na kiungo mshambuliaji, Never Tigere, huku mshambuliaji Obrey Chirwa, aliyekuwa mgonjwa naye akianza mazoezi.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kuinyuka Mbao mabao 2-0, yaliyofungwa na washambuliaji Shaaban Chilunda na Richard Djodi, huku Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita.

Back to Top