Mechi ya Kirafiki | Azam FC, KMC zatoka sare

Category: 
Team: 
Azam FC

KLABU ya Azam imemaliza programu ya mechi za kirafiki kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex jana Jumatano usiku.

Mchezo huo ni wa pili wa kirafiki baada ya ule wa awali dhidi ya Transit Camp kuisha kwa suluhu, ambapo Azam FC imezitumia mechi hizo kujiandaa na urejeo wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC itaanza patashika za ligi kwa kuchuana na Mbao, mtanange utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumapili hii saa 1.00 usiku.

KMC ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Serge Tape dakika 55 kabla ya Azam FC kusawazisha kwa bao lililofungwa na kiungo, Mudathir Yahya, dakika ya 80.

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, limefurahishwa na ushindani wa mechi zote mbili za kirafiki walizocheza, ambapo kocha huyo amejipanga kurekebisha makosa yote kabla ya kucheza na Mbao.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea kubakia kambini na leo Alhamisi jioni kitaendelea na mazoezi kama kawaida tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kurejea kwa patashika ya ligi.

Hadi sasa kikosi cha Azam FC kinawakosa jumla ya wachezaji nane wa kigeni, mshambuliaji Obrey Chirwa, akiwa mgonjwa huku kipa Razack Abalora, mabeki Daniel Amoah, Yakubu Mohammed (Ghana), beki wa kushoto Bruce Kangwa, kiungo Never Tigere, mshambuliaji Donald Ngoma (Zimbabwe) na Mganda Nickolas Wadada, wakiwa wamekwama katika nchi zao baada ya mipaka kufungwa.

Back to Top