Match Report: Yanga SC 0-0 Azam FC

Category: 
Team: 
Azam FC

KLABU ya Azam imeendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kutoka suluhu na mpinzani wake katika nafasi hiyo Yanga.

Suluhu hiyo imeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 58 huku Yanga nayo ikijiongezea pointi moja baada ya kufikisha 56, na Simba iliyo kileleni ikiwa nazo 75.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ulishuhudiwa ukiwa na matukio kadhaa tata kwenye uamuzi yaliyofanywa na waamuzi waliouchezesha, akiwemo wa kati, Heri Sasii.

Mwamuzi msaidizi namba moja, Soud Lila, dakika ya pili ya mchezo, alianza kulikataa bao la beki wa kati wa Azam FC, Abdallah Kheri, alilofunga kwa kichwa akimalizia krosi ya winga Idd Seleman ‘Nado’, mwamuzi akidai mfungaji alikuwa ameotea.

Tukio kama hilo lilijirejea dakika ya 47 ya mchezo, kwa bao jingine la Azam FC kukataliwa, lililofungwa na kiungo mshambuliaji, Never Tigere, akiunganisha pasi ya Nado, na mwamuzi akadai mfungaji alikuwa ameotea.

Mbali na Azam FC kunyimwa mabao hayo, pia ilinyimwa penalti ya wazi dakika ya 76, baada ya beki wa kulia Nickolas Wadada, kuangushwa kwa makusudi ndani ya eneo la hatari na beki wa Yanga, Jaffari Mohamed, lakini mwamuzi Sasii, akaonekana kupeta licha ya kuwa karibu na eneo la tukio.

Aidha licha ya kunyimwa mabao hayo, Azam FC ilipoteza nafasi kadhaa za wazi za kufunga mabao kupitia kwa wachezaji wake Idd Kipagwile, aliyepoteza mbili Richard Djodi na Shaaban Chilunda na kufanya matokeo yamalizike kwa suluhu hiyo.

Kipa wa Azam FC, Benedict Haule, alionekana kuwa nyota wa mchezo baada ya kuokoa michomo mingi ya hatari ya wachezaji wa Yanga, huku safu ya ulinzi chini ya Abdallah Kheri, Oscar Masai, Wadada na Salmin Hoza, nayo ikionekana kufanya vizuri.

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kujizolea pointi nne kwenye mechi mbili ilizocheza dhidi ya Yanga msimu huu, baada ya mechi ya kwanza kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kucheza mechi mbili zijazo ugenini, dhidi ya Kagera Sugar Juni 24 na Biashara United Juni 27.

Back to Top