Match Report: Azam FC 2-0 Mbao

Category: 
Team: 
Azam FC

KLABU ya Azam FC imeendelea pale ilipoishia kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Mbaoa mabao 2-0 jana Jumapili usiku.

Kabla ya ligi hiyo kusimamishwa Machi 17, mwaka huu kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, Azam FC iliichapa Ruvu Shooting mabao 2-1, yote yakifungwa na kiungo mshambuliaji, Never Tigere.

Azam FC kwa ushindi wa jana imefikisha jumla ya pointi 57 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa nyuma pointi 17 dhidi ya Simba inayoongoza kileleni yenye pointi 72.

Wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex, waliozizindua nyasi mpya za uwanja wake huo katika mechi ya kwanza ya mashindano, walionyesha kiwango kizuri cha usakataji kabumbu hasa kipindi cha pili cha mchezo huo.

Kipindi cha kwanza walifanikiwa kutengeneza nafasi takribani nne za kufunga mabao, nafasi mbili kati ya hizo zikiwahusisha winga Idd Seleman ‘Nado’ na mshambuliaji Andrew Simchimba, waliogongesha miamba kutokana na mashuti waliopiga.

Kipindi cha pili Azam FC ilibadilika na kucheza soka la kasi na kulishambulia vilivyo lango la Mbao, ikitaka kupata bao la mapema ili kuimaliza mechi hiyo

Hatimaye dakika ya 49, pasi za mgongeano walizopigiana kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, winga Idd Kipagwile na Idd Seleman ‘Nado’, zilizaa matunda kwa bao safi lililofungwa kwa kisigino na mshambuliaji Richard Djodi, akimalizia pasi ya mwisho ya Nado.

Mshambuliaji Shaaban Chilunda, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Simchimba, aliipatia bao la pili Azam FC dakika ya 90 akimalizia pasi safi ya Nahodha wa mchezo huo, ambaye ni msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kukipiga dhidi ya Yanga kwenye mchezo ujao wa ligi, utakaofanyika Uwanja wa Taifa Jumapili ijayo Juni 21 mwaka huu.

Back to Top