Match Preview: Simba v Azam FC

Category: 
Team: 
Azam FC

NI mpambano wa kufa au kupona! Ndio unavyoweza kuielezea hivyo mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) kati ya Azam FC na Simba, itakayofanyika kesho Jumatano saa 1.00 usiku.

Mtanange huo mkali unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini, utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, ukitarajia kuamua ni timu ipi kati ya Azam FC na Simba itatinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo, mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2017, katika hatua ya nusu fainali, Azam FC ikipoteza kwa bao 1-0, mechi iliyogubikwa na utata mkubwa baada ya mwamuzi wa mchezo huo Mathew Akrama, kumtoa kwa kadi nyekundu yenye utata kiungo Salum Abubakar.

Vijana wa Azam FC wapo katika hali nzuri kabisa kuelekea mchezo huo, wakiwa na morali ya hali ya juu kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kutinga nusu fainali na baadaye fainali ili kutetea taji hilo, walilolitwaa msimu uliopita kwa kuichapa Lipuli bao 1-0.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, akizungumza kuelekea mtanange huo amesema anaiheshimu Simba kutokana na ubora wa kikosi walichokuwa nacho, lakini amekipanga kikosi chake kupambana kufa au kupona kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mchezo huo.

“Timu yetu kesho inahitaji kufanya uamuzi na kujipanga vizuri kwenye uwanja, kwa sababu tunacheza na timu moja nzuri, pia wachezaji wanatakiwa kufahamu waende kucheza kwa moyo na kujitoa, kwa sababu ni mechi moja tu ya FA na timu moja itatoka, nahitaji kesho wachezaji wangu wajitoe uwanjani ili kupata matokeo mazuri,” alisema.

Nao manahodha wa kikosi hicho, nahodha mkuu Agrey Moris na Msaidizi wake, Frank Domayo ‘Chumvi’, wamejinasibu ya kuwa wataingia uwanjani kupambana na kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

“Tunajua tunaenda kukutana na mechi ngumu na mechi hiyo itakuwa ni mechi nzuri kwa pande zote mbili, mimi naimani mchezo huo mtu anahitaji kuwa makini, atakayefuata maelekezo ndio atakayepata matokeo katika mchezo huo,” alisema Moris.

Domayo aliongezea kuwa; “Tumekaa kwa pamoja wachezaji kama wachezaji tumeelezana hali halisi ilivyo kikubwa kwamba mwalimu pia katupa mbinu, mazoezi ya siku mbili hizi zote ni kwa ajili ya umaliziaji, kikubwa tuamke vizuri siku hiyo tuweze kupambania ushindi.”

Ushindi wowote wa Azam FC utaifanya kusonga mbele kwa hatua ya nusu fainali, ambapo itakutana na mshindi wa robo fainali nyingine kati ya Yanga na Kagera Sugar.

Bingwa wa mchuano hiyo anatarajia kutwaa kombe na kitita cha Sh. Milioni 50, huku pia akitarajia kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Back to Top