Kocha Azam FC aomba wachezaji wa akiba waongezwe

Category: 
Team: 
Azam FC

KOCHA Mkuu wa klabu ya Azam FC, Aristica Cioaba, ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongeza idadi ya wachezaji wa akiba kutoka watatu hadi watano.

Cioaba ametoa ombi hilo kwa TFF, akiwa na malengo ya kuwasaidia wachezaji kujiepusha na majeraha, endapo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itarejeshwa hivi karibuni.

Ligi hiyo kwa sasa imesimamishwa kwa muda wa mwezi mmoja tokea Machi 17 mwaka huu, kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) linaloendelea kuitesa dunia, lakini mpaka sasa haijajulikana kama itarejea baada ya muda huo wa mwezi mmoja kuisha.

“Nadhani ninachosema ni ukweli halisia, narudia tena hili ni pendekezo langu binafsi endapo wataamua kurudisha ligi mwezi ujao au miezi miwili ijayo, nadhani itakuwa jambo la busara kuongeza idadi ya wachezaji wanaofanyiwa mabadiliko kutoka watatu hadi watano.

“Namna nyingine ni kurahisisha kazi kwa makocha na wachezaji, katika mazingira haya ni kuongeza idadi ya wachezaji wa akiba kutoka saba hadi tisa…ili kuwasaidia,” alisema Cioaba alipozungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kutoka nchini kwao Romania.

Kocha huyo raia wa Romania mwenye leseni ya juu ya ukocha ya Baraza la Vyama vya Soka Ulaya (UEFA Pro Licence), aliongeza kuwa; “Unajua siyo wachezaji wote watakuwa timamu kimwili kwa asilimia 10, kwa hiyo tukifanya hivi tutakuwa tunawaepusha na majeraha.”

Aidha alisema anamuomba Mwenyezi Mungu atusaidie tupite salama katika kipindi hiki kigumu, huku akiwatakia Watanzania wote afya njema pamoja na kuchukua tahadhari za ugonjwa huo.

Back to Top