Kipre Tchetche: Nina furaha kubwa Azam FC

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Kipre Tchetche, amesema kuwa bado anafuraha kubwa ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati.

Kauli ya nyota huyo imekuja baada ya kutoka taarifa mbalimbali zinazomuhusisha Tchetche kujiunga na Yanga katika dirisha hili dogo la usajili.

“Kiukweli sijawahi kuwasiliana au kuwa na namba ya kiongozi au mtu yoyote wa Yanga, mawazo yangu yote yapo kwenye timu yangu hii kwani bado nina mkataba na ninafuraha kubwa kuwa hapa.

“Sitaki kuchanganya mambo mengine yoyote na mimi mwenyewe pia kujichanganya, nataka kuisaidia zaidi timu yangu,” alisema nyota huyo kutoka nchini Ivory Coast wakati akizungumza na mtandao huu wa azamfc.co.tz

Kabla ya Tchetche kutoa kauli hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alishaweka wazi kuwa wamekuwa wakisikia kwenye vyombo vya habari kuhusu mchezaji huyo kutakiwa pamoja na Pascal Wawa, lakini wao kama uongozi hawajapokea barua yoyote rasmi mpaka sasa.

Tchetche, 28, amefanya vizuri mpaka kwenye msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), akiwa amefunga mabao saba katika mechi tisa ilizocheza Azam FC.

Mabao hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri kwa Azam FC, ambayo mpaka sasa ipo kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 25 ikishinda mechi nane na sare moja.

 

Back to Top