Kapombe apewa tuzo yake ya Mchezaji Bora

BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC na Taifa Stars, Shomari Kapombe, leo asubuhi amekabidhiwa mfano wa hundi ya Sh. milioni moja baada ya mwezi uliopita kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kapombe alikabidhiwa hundi hiyo na mwakilishi kutoka wadhamini wakuu wa ligi hiyo Kampuni Vodacom, Ibrahim Kaude, ambaye ni Afisa Matukio na Udhamini wa Vodacom, aliyeambatana na Afisa wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), Joel Barisidya.

Beki huyo wa kutumainiwa alitwaa tuzo hiyo kwa kuwapiku nyota wawili alioshindanishwa nao, mshambuliaji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Jeremiah Juma na beki wa Coastal Union ya Tanga, Miraji Adam.

Siri ya mafanikio yake?

“Cha kwanza mimi naweza kusema siri kubwa ya mimi kufanikiwa ni kujituma nje na ndani ya uwanja, cha pili kumsikiliza kocha anasemaje na anahitaji nini, cha tatu ni kuwa na mahusiano mazuri na wachezaji wenzangu na cha nne ni kujitolea uwanjani ili kuifanya timu yangu ifike sehemu nzuri na mimi kuonekana niko bora zaidi,” alisema Kapombe alipokuwa akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz hivi karibuni.

Amefanya nini msimu huu?

Kapombe anayesifika kwa soka la kasi akipanda na kushuka katika majukumu yake ya ulinzi na kusaidia ushambuliaji (wingback) upande wa kulia na wakati mwingine kushoto, mbali na kufanikiwa kutoa pasi nyingi za mwisho msimu huu pia amefunga mabao nane kwenye ligi.

Hilo limemfanya kuwa beki pekee kufunga mabao mengi kwenye ligi hiyo huku akiwa mmoja wa wafungaji bora ndani ya Azam FC msimu huu sambamba na Kipre Tchetche (9) na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ (8).

Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, pia ameshafunga bao moja mpaka sasa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, alilofunga wakati wakiilaza Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 3-0 jijini Johannesburg.  

Back to Top