Kangwa, Tigere watia ‘timu’ Azam FC

Category: 
Team: 
Azam FC

KIKOSI chetu cha Azam FC kinazidi kukamilika, baada ya kuwapokea wachezaji wawili kutoka Zimbabwe, beki wa kushoto, Bruce Kangwa na kiungo mshambuliaji, Never Tigere leo Jumatatu Juni 15 mwaka huu jioni.

Wachezaji hao walikuwa wamekwama nchini kwao Zimbabwe kutokana na vikwazo vya ugonjwa wa virusi vya Corona, lakini jitihada za uongozi wa Azam FC zimefanikisha wawili hao kuwasili nchini.

Nyota hao wamepokelewa na Meneja wa timu hiyo, Luckson Kakolaki, ambapo kesho Jumanne wanatarajia kujiunga rasmi mazoezini pamoja na wachezaji wengine wa timu hiyo.

Azam FC inazidi kukamilika, wakati huu ikiwa kwenye harakati za kugombea taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) pamoja na kutetea ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), hivi sasa ikiwa imefika robo fainali na ikitarajiwa kucheza na Simba Julai Mosi.

Mara baada ya kuwasili, wachezaji hao wameahidi watajiweka sawa kwa ajili ya kuipigania timu hiyo katika michuano hiyo, ikiwemo kuhakikisha wanatetea ubingwa wa FA.

Tigere na Kangwa wanawasili, wakati Azam FC ikitoka kuichapa Mbao mabao 2-0 kwenye muendelezo wa mechi za ligi, ambapo Jumapili hii kikosi cha Azam FC kitashuka dimbani kupambana na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji pekee ambao bado hawajawasili nchini kuungana na wenzao kumalizia mechi za ligi na Kombe la FA (ASFC), ni Waghana, kipa Razack Abalora, mabeki wa kati, Daniel Amoah na Yakubu Mohammed.

Back to Top