Farid atua salama Hispania

WINGA machachari wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, tayari ameshafika salama jijini Madrid Hispania leo, kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu ya huko ‘La Liga’.

Klabu hizo atakazofanyiwa majaribio ni Malaga inayoshika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi hiyo pamoja na Las Palmas iliyopo nafasi ya nane wakiwa na pointi 43.

Farid atakaa huko kwa takribani wiki tatu na anatarajia kurejea nchini Mei 19 mwaka huu, hiyo inamaanisha kuwa ataukosa mechi zote zilizobakia za msimu huu za Azam FC.

Winga huyo, 20, atakuwa na wakala wake kwa kipindi chote atakachotumia akiwa huko na ili uweze kupata taarifa za kina kuhusu maendeleo yake kwenye majaribio hayo tafadhali tembelea tovuti hii rasmi wa Azam FC (www.azamfc.co.tz).

Malaga ni moja ya timu bora kabisa kwenye La Liga kwani imewahi kuwatoa wachezaji wanaotamba hivi sasa Ulaya kama vile kiungo Isco wa Real Madrid, beki wa kushoto wa  Arsenal, Nacho Monreal na kiungo Santi Cazorla waliyemsajili kutoka Villareal kwa ada iliyovunja rekodi ya usajili kwa timu hiyo ya Euro milioni 21 kabla ya kuuzwa kwenda Arsenal, anayochezea mpaka sasa.

Kama Farid mambo yakimnyookea vema na kusajiliwa na moja ya timu kati ya hizo, atakuwa Mtanzania wa kwanza kucheza kwenye moja ya ligi kubwa tano zinazotamba duniani na huko atakutana na mastaa wanaotikisa ulimwengu kwa sasa katika soka, mchezaji bora wa dunia Lionel Messi (Barcelona) na Cristiano Ronaldo (Real Madrid).

Back to Top