BREAKING NEWS: Chirwa aongeza mwaka mmoja Azam FC

Category: 
Team: 
Azam FC

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Obrey Chirwa, ameongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kusalia ndani ya timu hiyo.

Mkataba wa awali wa nyota huyo alioongeza Juni mwaka jana, ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo kwa kusaini tena kutamfanya aendelee kusalia hadi mwishoni mwa msimu ujao.

Chirwa, aliyejiunga na Azam FC msimu uliopita amesaini mkataba huo mbele ya Afisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’.

Mara baada ya kusaini mkataba huo, Chirwa ameelezea kufurahishwa kuendelea kusalia ndani ya timu hiyo, huku akiahidi kufanya vizuri zaidi.

“Nawaomba mashabiki huu mwaka kwangu nishafanya vizuri, nitaendelea kufanya vizuri na mwaka huu 2020 nitaendelea kuwafurahisha mashabiki wa Azam nawaomba tu uwanjani waje kwa wingi,” alisema.

Mshambuliaji huyo raia wa Zambia, amekuwa na msimu mzuri hadi sasa akiwa kinara wa upachikaji wa mabao Azam FC, hadi sasa akiwa ameshafunga jumla ya mabao 11 kwenye michuano yote.

Miongoni mwa mabao hayo, Chirwa kwenye ligi amefunga nane, Kombe la Mapinduzi mawili na moja katika michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika jijini Kigali, Rwanda, akiisaidia Azam FC kumaliza nafasi ya pili kwenye michuano hiyo.

Back to Top