Azam FC, TFF kuadhimisha siku ya utoaji damu duniani

Category: 
Team: 
Azam FC

KLABU ya Azam kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa pamoja wataadhimisha siku ya utoaji damu duniani keshokutwa Jumapili Juni 14 mwaka huu.

Azam FC siku hiyo itakuwa kicheza mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mbao saa 1.00 usiku, ambapo zoezi la uchangiaji damu litafanyika nje ya viunga vya Azam Complex kuanzia saa 6 mchana.

Ushirikiano huo kati ya Azam FC na TFF, utanogeshwa na mchezo wa kirafiki, utakaohusisha wafanyakazi wa timu hizo, utakaofanyika saa 2.00 asubuhi, kabla ya Azam FC haijacheza na Mbao.

“Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeona kuna haja ya kushirikiana na Azam FC katika kuadhimisha siku ya utoaji damu Kimataifa siku ya tarehe 14 Juni 2020,” ilisema taaraifa iliyotolewa na TFF.

Utaratibu mzuri umeandaliwa kwa watu wote wataojitokeza kuchangia damu, ambapo watazawadiwa tiketi ya bure kushuhudia mechi kati ya Azam FC na Mbao.

Azam FC, tunatoa wito kwa watu mbalimbali wakiwemo mashabiki wote, kujitokeza kwa wingi kusapoti juhudi za Serikali pamoja na Kitengo cha Damu Salama, katika kutunisha benki ya damu ya Taifa, ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu wenye uhitaji wa damu hospitalini.

Back to Top