‘Wachezaji wanafurahia kuchezea Azam Complex'

Category: 
Team: 
Azam FC

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amesema kuwa wachezaji wake hivi sasa wanafurahia kucheza kwenye nyasi mpya za Uwanja wa Azam Complex.

Cioaba ametoa kauli hiyo baada ya mechi ya kwanza ya timu hiyo ndani ya nyasi hizo mpya dhidi ya Transit Camp, iliyofanyika jana Jumamosi usiku na kuisha kwa suluhu.

“Nilikuwa na mazoezi hapa ya wiki moja wakati mwingine wachezaji wengine hawauelewi uwanja, juu ya utofauti huu ni uwanja mpya inahitaji kuuzoea, lakini pia wapinzani nao imekuwa hali hiyo, uwanja ni mzuri wachezaji wanapenda kucheza mechi kwenye uwanja wetu wa nyumbani (Azam Complex),” alisema.

Akizungumzia mchezo huo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Transit Camp, Cioaba amekiri kuona mapungufu kwa baadhi ya wachezaji wake, huku akisema anahitaji kuifanyia kazi sehemu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

“Tatizo ni lile lile, umeona tumepata nafasi tatu au nne za kufunga mabao kipindi cha kwanza na hatukuweza kufunga na hali hiyo hiyo ilitokea huko nyuma kabla ya kipindi hiki cha Corona, tulikuwa tukipata nafasi nyingi za kufunga na hatukuweza kuzitumia nafasi hizo, hali hiyo imeendelea tena, nahitaji kulifanyia kazi kwa viungo washambuliaji na washambuliaji kwa ajili ya kumaliza tatizo hili,” alisema.
Alisema amefurahishwa na wachezaji namna walivyoingia kwenye mchezo huo huku akiwakumbuka nyota wake nane wa kigeni wanaoendelea kukosekana kikosini.

“Nina furaha kwa kuwa baadhi ya wachezaji waliingia uwanjani na nikaona wakiwa vizuri fiti lakini sio wachezaji wote, wachezaji watatu au wanne walikuwa vizuri ndani ya uwanja wakiwa fiti, walicheza wachezaji wengi vijana kutokana na hii hali, wachezaji wetu saba wa kigeni haiwezekani kuja kwa sababu bado viwanja vyao vya ndege vimefungwa.

“Nimejaribu baadhi ya wachezaji kutoka timu ya vijana, nimejaribu baadhi ya wachezaji kucheza nafasi mpya lakini tunahitaji kufanya kazi tena kwa muda wa wiki moja, nina mechi nyingine ya kirafiki Jumatano (ijayo) na labda hatua kwa hatua watafika juu, siku saba pekee hazitoshi kufanya kazi pamoja na mechi ya kwanza ya kirafiki kila mmoja ndani ya uwanja acheze vizuri,” alisema.

Wachezaji saba wa kigeni wa Azam FC, ambao bado hawajarejea nchini kutokana na changamoto za ugonjwa wa virusi vya Corona iliyofanya mipaka ya nchi zao kufungwa, ni waghana Razack Abalora, Daniel Amoah, Yakubu Mohammed, Wazimbabwe Bruce Kangwa, Never Tigere, Donald Ngoma pamoja na Mganda Nickolas Wadada.

Kocha huyo bora wa ligi mwezi mwezi Novemba na Januari msimu huu, alikiri kuwakosa wachezaji hao saba akiwemo Obrey Chirwa ambaye ni mgonjwa, ni pigo kwa kikosi chake kutokana na umuhimu wa baadhi ya wachezaji hao, huku akidai anajipanga kukabiliana na hali hiyo kwa kuandaa wachezaji waliopo kikosini.

Azam FC itaanza rasmi kukipiga dhidi ya Mbao kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Juni 14 mwaka huu saa 1.00 usiku.

Back to Top